Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kushirikiana na Korea Kusini kuandaa wataalamu wa Tehama

Technology Serikali kushirikiana na Korea Kusini kuandaa wataalamu wa Tehama

Tue, 7 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kutokana na mabadiliko ya ulimwengu, Serikali imesema inafanya kila namna kuhakikisha inawaandaa wanafunzi kusoma taaluma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Hatua hiyo inatokana na kile kilichoelezwa, mabadiliko ya sera ya elimu iliyoridhiwa hivi karibuni, yanahimiza matumizi ya Tehama katika ujifunzaji na ufundishaji.

Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imesaini mkataba wa makubaliano na Ofisi ya Elimu ya Gwangju Metropolitan (GMOE) ya Korea Kusini, kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ushirikiano wa maboresho ya ujifunzaji na ufundishaji wa Tehama.

Akizungumza katika hafla ya kusainiwa kwa makubaliano hayo leo, Novemba 7, 2023, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe amesema Serikali inafanya kila namna kuhakikisha inaandaa wanafunzi watakaosoma Tehama.

Amesema makubaliano hayo ni sehemu ya jitihada hizo na kwamba yatawajengea walimu na wanafunzi uwezo kuhusu Tehama, kulingana na matakwa ya ulimwengu wa sasa.

"Natoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Korea Kusini kwa msaada inayoendelea kutoa katika kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya Tehama," amesema.

Kuhusu makubaliano hayo, Profesa Mdoe amesema yatahusisha kutoa mafunzo kazini kwa walimu, utoaji wa vifaa vya Tehama vya kujifunzia na kufundishia na kubadilishana wataalamu kwa wanafunzi na walimu wanaojitolea kati ya Tanzania na Korea Kusini.

Ameleza hiyo itasaidia walimu kuwa na mtazamo chanya katika Tehama na mafunzo yake.

Hata hivyo, amesema hiyo ni awamu ya pili ya makubaliano hayo kwani ya awali yalifanyika mwaka 2021 yakihusisha msaada wa vifaa mbalimbali vya Tehama katika shule mbili nchini ambazo ni Tegeta A na Kimbiji.

"Utekelezaji wa makubaliano haya utahusisha mafunzo kwa walimu ili kuwaandaa kutekeleza sera mpya na kwamba vifaa vya Tehama vitawezesha kutimiza azma ya Serikali na mwanzo mzuri wa kutekeleza mitalaa hiyo.

"Mashirikiano haya yamekuja wakati muafaka kwa sababu yatatusaidia kupanda mbegu ya matumizi ya Tehama katika kujifunza na kufundishia na utaalamu wa Tehama kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na hatimaye kuwaandaa vema kujifunza mafunzo hayo," amesema.

Amesema katika Karne ya 21 matumizi ya Tehama ni muhimu kwa maendeleo ya elimu na yanaboresha ujifunzaji.

Amesema matarajio ya Serikali ni kuwepo mwendelezo kwa maana ya kwenda katika shule zaidi ya mbili ambazo makubaliano hayo yanajihusisha nazo.

Amewataka wakuza mitalaa na watakaofaidika na mafunzo hayo wasaidie namna ya kuwezesha Tehama itumike zaidi kwenye kufundisha na kujifunza kwa ngazi zote za elimu.

Akizungumza mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk Aneth Komba amesema kwa mara ya kwanza makubaliano hayo yalisainiwa mwaka 2021.

Amesema shabaha yake ni kuimarisha matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) katika ujifunzaji na ufundishaji.

Yapo maeneo matatu, kwa mujibu wa Dk Aneth yatakayohusika na makubaliano hayo, ikiwemo Ofisi ya Guanju Metropolitan kuipa TET vifaa vya Tehama.

"TET itawajibika kulipia gharama za ugomboaji wa vifaa hivyo bandarini na kuvisafirisha katika shule husika," amesema.

Kadhalika, amesema makubaliano hayo yatahusisha ofisi hiyo kuandaa na kuwaalika walimu na watumishi wengine wa umma nchini Korea Kusini kwa mafunzo.

Amesema Ofisi ya Elimu ya Gwangju itatoa wataalamu kuja Tanzania kutoa mafunzo na itabeba gharama zote ikiwemo safari na malazi.

Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji, amesema jumla ya wataaluma 50 na walimu 40 kutoka Kimbiji na Tegeta A walipata mafunzo juu ya namna ya kuandaa, kutengeneza na kutumia maudhui ya kielektroniki katika ufundishaji na ujifunzaji.

"Baada ya mafunzo hayo TET ilipatiwa kompyuta 50, spika 52, webu kamera 50, UPS 52, tableti 40, skana 2, printa 2, projekta 2, majukwaa ya kidijitali 2, skrini za projekta 2, vipanya visivyo na waya 50, keybody 50, hedifoni 52, na vingine vingi.

Kwa upande wa shule, kila shule ilipokea kompyuta 25, spika 26, webu kamera 25, UPS 26, tableti 20, skana 1, printa 1, projekta 1, majukwaa ya kidijitali 1, ubao wa kielektroniki 1, vipanya visivyo na waya 35, vipanya vyenye waya 25, kiibodi 25, hedifoni 26, adapta 49, na USB flash drives 50," amesema.

Amesema vifaa hivyo vimetumika kuanzisha maabara za Kompyuta katika shule husika na zimeleta mapinduzi katika ufundishaji na ujifunzaji.

Amesema mradi huo kwa mwaka huu utahusisha shule ya Msingi Mkombozi na Shule ya Sekondari Mabatini zote za Mkoa wa Njombe.

Ameeleza tayari TET imeshapokea vifaa mbalimbali vya Tehama kwa ajili ya shule hizo.

Gavana wa Guanju Metropolitan, Lee Jeong amesema elimu ndilo tumaini na ndiyo chanzo cha mafanikio kwa siku za baadaye.

Ili kufikia maendeleo, amesema ni muhimu watu wa taifa husika wawe na ari ya kujifunza, akidokeza ndiyo mbinu ambayo Korea Kusini imeitumia kufanikiwa.

"Kwa kuwa wananchi walikuwa na ari ya kutaka kufika tulipofika sasa, ndiyo iliyoifanya Korea kufikia ilipofika," amesema.

Na katika ari hiyo, Jeong amesema ni vema kuwa na ndoto na kuwa na nchi ya mfano wa mafanikio.

"Ni vema kuwa na ndoto na kutafuta namna ya kuitimiza na njia moja ni kumtafuta mtu wa mfano ambaye tayari ametimiza ndoto yake," amesema.

Amesema ni muhimu nchi kuwa na mitalaa mizuri itakayowezesha mafunzo ya Tehama kwa kuwa ndiko ulimwengu unakoelekea.

Si hivyo tu, amesema hayo yote yanapaswa kuendana na uwepo wa walimu wenye uwezo wa kutumia na kufundisha vema Tehama.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live