Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kusambaza mchele nchi jirani

Mchele Nchi Jirani Serikali kusambaza mchele nchi jirani

Fri, 3 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imekamilisha mikakati ya kuliwezesha taifa kuwa kitovu cha kuwezesha mataifa mengine jirani kupata mchele wa kutosha ifikapo mwaka 2030.

Tanzania ambayo ni taifa la nne kwa uzalishaji wa mpunga Afrika na ya pili kwa mataifa ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, imekuwa na ongezeko la mauzo ya mchele katika miaka mitatu iliyopita ikidhihirisha kukua kwa kilimo hicho.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya kilimo cha mpunga, Anna Mwangamilo wa Wizara ya Kilimo alisema kwa sasa nchi imejitosheleza kwa mchele na kwamba sasa wakulima wanaendelea kuzalisha kwa ajili ya biashara.

Alisema kuanzia mwaka 2020 uzalishaji wa mchele nchini umekuwa ukipanda kiasi cha taifa kujitosheleza na kuanza kuuza nje. Alisema mipango iliyopo ni taifa kuwa kitovu cha kuwezesha mataifa mengine jirani kupata mchele wa kutosha ifikapo mwaka 2030.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni kubadili mfumo wa kilimo na kuwa wa kutegemea teknolojia kwa matumizi ya zana za kisasa, mbegu za kisasa na kilimo cha umwagiliaji.

Utekelezaji wa mkakati huo kati ya serikali na sekta binafsi kutaleta ushindani utakaowezesha kufikia makadirio ya uzalishaji wa tani milioni 8.8 za mchele ifikapo 2030.

Kwa mujibu wa Anna, msaada ulielekezwa kwa mradi wa uzalishaji mchele wa Afrika Mashariki (CARI-EA), uliotolewa na USAID na AGRA umekuwa msaada mkubwa wa kushawishi tija nchini.

“Mwaka 2021, Tanzania iliimarisha nafasi yake ya kuwa nchi inayoongoza kwa uzalishaji na uuzaji nje wa mchele katika nchi za Afrika Mashariki. Ina maana mchele wetu umekuwa na ushindani mkubwa katika ubora na bei kuliko uagizaji wa bidhaa kutoka nchi za Pakistani ambazo zilikuwa zikitishia mapato ya wakulima wadogo.

"Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuuza mchele nje ya nchi. Matokeo ya mpango wa CARI-EA yanaonyesha Tanzania inaweza kuongezeka kwa kiasi kikubwa kuuza mchele nje ya nchi," alisema Meneja wa AGRA nchini, Vianey Rweyendela.

Mpango wa CARI-EA, unaotekelezwa na Kilimo Trust, umeonesha kuwa juhudi za pamoja katika sekta ndogo ya mpunga zinaweza kuongeza ushindani wa mchele unaozalishwa nchini.

Katika mpango huo kulipatikana vikundi 12 vya biashara ya mpunga vinavyohudumia wakulima wadogo wapatao 150,000 na kifurushi cha kazi ya ugani unaoongozwa na mtu binafsi, kuwezesha soko.

Mpango huu umejikita katika mikoa saba ya Tanzania Bara ambayo ni Simiyu, Shinyanga, Morogoro, Mbeya, Iringa, Rukwa na Katavi pamoja na Unguja na Pemba.

Mratibu wa mradi katika AGRA, Japhet Laizer, alisema wakulima waliwezeshwa na huduma za maendeleo ya biashara hali iliyosababisha kuongezeka kwa uzalishaji na upatikanaji wa soko.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live