Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kurahisisha usafiri Bandari Bagamoyo

Bandari Bagamoyo Serikali kurahisisha usafiri Bandari Bagamoyo

Sat, 9 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

SERIKALI imesema itajenga gati kwenye Bandari ya Bagamoyo kwa ajili ya kurahisisha usafiri kutoka bandarini hapo kwenda Zanzibar ili kuvutia watalii. Hayo yalisemwa Bagamoyo na Naibu Waziri Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete baada ya kutembelea eneo litakapojengwa gati hilo.

Aliitaka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kupeleka wataalamu wiki ijayo wafanye usanifu wa ujenzi wa gati. Mwakibete alisema kuwa kumekuwa na changamoto ya ukosefu wa boti za kisasa kati ya Bagamoyo na Zanzibar kwa ajili ya abiria pamoja na mizigo na hasa watalii.

Kwa mujibu wa naibu waziri, Zanzibar inapokea watalii 300,000 kwa mwaka huku Bagamoyo ikipata watalii 27,000. “Naagiza TPA ilete wataalamu Jumanne ya wiki ijayo waje hapa kuja kupima na kuleta wizarani makadirio kwa ajili ya ujenzi wa gati ili boti na majahazi yaweze kuja na kwenda Zanzibar,” alisema Mwakibete.

Alisema kuwa kazi ya wizara ni kuwezesha miundombinu na Bagamoyo ni mji wa kitalii hivyo miundombinu ikiwa mizuri watalii wengi watafika baada ya kutembelea Zanzibar. “Gati likijengwa hapa, utalii utakua kwani watalii wengi wanapenda kuja Bagamoyo wakitokea Zanzibar lakini wanashindwa kutokana na kutokuwa na usafiri wa uhakika wa majini hasa ikizingatiwa hapa na Zanzibar ni karibu sana,” alisema Mwakibete.

Ombi la ujenzi wa gati linatajwa kuchochewa zaidi baada ya uongozi wa Wilaya ya Bagamoyo kwenda Zanzibar kwa ajili ya Royal Tour na kuona walivyofanikiwa kwenye sekta ya utalii. Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete alisema uwapo wa gati utafungua kiuchumi Wilaya ya Bagamoyo na kuondoa bandari bubu ambazo ni nyingi na kusababisha watu kufanya biashara za magendo.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Abdala alisema kampuni za Bahressa na Songoro Marine zimeonesha nia ya kupeleka boti endapo gati litajengwa. Mbunge wa Bagamoyo, Muharami Mkenge alisema bandari hiyo sasa inaingiza Sh bilioni 27 kwa mwaka hivyo kujengwa kwake kutaongeza mapato zaidi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live