Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kuongeza watumiaji huduma za kifedha

FEDHA WEB Serikali kuongeza watumiaji huduma za kifedha

Mon, 20 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imesema kwa sasa kuna asilimia 53.8 ya Watanzania ambao ndiyo wamefikiwa na huduma rasmi za kifedha ikiwemo benki na huduma nyingine.

Kutokana na idadi hiyo Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha, imepanga hadi ifikapo mwaka 2025, asilimia 80 ya Watanzania wawe wamefikiwa na huduma hizo kwa kutoa elimu ya umuhimu wa matumizi ya huduma hizo.

Hayo yameelezwa leo Jumapili Novemba 19, 2023 na Kamishna wa Idara ya uendelezaji sekta ya Fedha, Dk Charles Mwamwaja, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya wiki ya huduma za fedha kitaifa, yanayotarajiwa kuanza kesho katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Dk Mwamwaja amesema kupitia utafiti walioufanya hivi karibuni ulionyesha bado asilimia kubwa hawatumii mifumo rasmi ya kifedha.

"Takwimu zinaonyesha bado idadi kubwa ya watanzania hawajafikiwa na huduma rasmi za kifedha, mpaka sasa kwa utafiti ambao tumeufanya hivi karibuni unaonyesha asilimia 53.8 ndiyo ambao wamefikiwa na huduma za fedha rasmi,"amesema Kamishna.

"Utaona bado tuna pengo na tuna kazi kubwa, ndiyo maana serikali imelenga ifikapo 2025,kuhakikisha asilimia 80 iweze kuwa imefikiwa na huduma rasmi," amesema.

Ameaema maadhimisho hayo ya tatu yatashirikisha wadau mbalimbali wa fedha ikiwemo benki 35, yana ajenda kuu ambayo ni kutoa elimu ili wananchi waweze kutumia huduma za kifedha kwa namna sahihi ikiwemo kutambua na kutumia fursa ambazo zinapatikana katika huduma hizo.

"Tunaposema huduma rasmi ni zile ambazo zinahusisha mifumo rasmi ya kifedha mfano anayetumia huduma za benki, masoko ya dhamana za mitaji, huduma za bima, huduma za mifuko uwezeshaji wananchi kiuchumi hizo ndizo ambazo tunasema huduma rasmi kutokaa na faida mbalimbali ambazo huduma hizo zinatoa," amesema na kuongeza:

"Kama mtu anaficha, anahifadhi fedha zake ndani kwenye godoro, mtungi na vihenge hizo siyo huduma rasmi na sehemu ya ajenda kubwa ambayo tunakusudia ni kutoa elimu kwa umma watu waweze kuona hatari ya kufanya hivyo lakini faida ambazo wanaweza kuzipata kwa kutumia huduma rasmi za kifedha."

Amesema kuwa maadhimisho hayo yanayoandaliwa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha watatoa elimu kuhusu usimamizi wa fedha binafsi, kutoa elimu kuhusiana na uwekaji akiba kuanzi ngazi ya mtu binafsi, vikundi na nyingine.

Kamishna huyo ameongeza kuwa maonyesho hayo yenye kauli mbiu isemayo ‘elimu ya fedha msingi wa maendeleo kiuchumi’ yatafunguliwa Novemba 22,2023 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Meneja Msaidizi wa mawasiliano kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Noves Mosses, amesema watatoa kwa makundi mbalimbali ya kijamii itakayowasiaidia kujiinua kiuchumi.

"Unapokuwa na elimu sahihi ya fedha utaua fursa zilizopo katika maeneo mbalimbali na ukitumia vizuri fursa hizo itasaidia kujiletea maendeleo kiuchumi,"amebainisha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live