Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kuongeza uzalishaji zao la kahawa

A12eedd5d081d5c174ca5e1f9ff432b2 Serikali kuongeza uzalishaji zao la kahawa

Thu, 8 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imetangaza hatua mpya zenye lengo la kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa nchini kutoka tani 50,000 zinazozalishwa sasa hivi kwa mwaka hadi tani 200,000.

Miongoni mwa hatua zinazochukuliwa ni kuanzisha mashamba makubwa ya pamoja yenye mashamba ya wakulima wadogo ndani yake.

Mpango huo mpya umelenga kuwezesha wakulima wadogo kuongeza tija na kuongeza uzalishaji kutoka tani 50,000 za kahawa kwa mwaka hadi tani 200,000, huku lengo halisi likiwa ni kufikia tani 300,000 kwa mwaka kama ilivyopendekezwa katika ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao katika Wizara ya Kilimo, Nyasebwa Enock alieleza hayo jana wakati wa kikao cha wadau wa kahawa kwamba mpango huo utawasaidia wakulima kupata huduma za ugani kwa urahisi kwa kuwa pamoja.

“Tumekuwa na uzalishaji mdogo kwa sababu ya utumiaji mdogo wa pembejeo za kilimo pamoja na miche bora, mbolea na viuatilifu. Tumegundua pia kutawanyika kwa wakulima kunachangia wao kutopata huduma za ugani,” alisema.

Enock alisema serikali inataka wakulima kutumia kikamilifu uwepo wa vyama vya ushirika ambavyo watavitumia kwa ajili ya kuagiza pembejeo za kilimo hasa mbolea na kuwauzia wanachama wake kwa bei ya chini.

Alisema vyama vya ushirika ni injini muhimu katika kukuza uzalishaji wa kahawa nchini na ndio maana serikali imekuwa ikivibana vyama vinavyofanya vibaya na hata kuvifuta.

Katika mwaka wa fedha 2019/20 serikali imefuta vyama vya ushirika 3,400 ili kuhakikisha kwamba vilivyobaki vinafuata taratibu na kusaidia wakulima.

Kulingana na mkurugenzi huyo, hatua nyingine ambazo zimechukuliwa kuimarisha upatikanaji wa masoko, huduma za kifedha na kuwezesha teknolojia kati ya wakulima wadogo.

Alisema wakulima wa kahawa wanachopaswa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba wanatumia teknolojia zilizopo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji na kuongeza tija.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Profesa Jamal Adam alisema bodi hiyo ina matumaini kuwa hatua mpya zitakazochukuliwa zitaongeza uzalishaji.

Alisema upatikanaji wa pembejeo za kilimo na matumizi bora ya kanuni za kilimo kunaweza kuongeza uzalishaji mara mbili kwa kutumia miti iliyopo.

“Tunaamini katika miaka mitano ijayo, tunaweza kuzalisha zaidi ya tani 200,000 za kahawa,” alibainisha.

Mwaka jana zao la kahawa lilichangia zaidi ya Dola za Marekani milioni 200 katika mapato ya fedha za kigeni kwa serikali na linabaki kuwa moja ya mazao mkakati ya biashara nchini.

Chanzo: habarileo.co.tz