Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kununua tani 100,000 za chakula

Kihenge Moja ya vihenge vya kuhifadhia mazao ya chakula

Tue, 31 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Huenda wakulima nchini Tanzania wakapata ahueni ya soko la uhakika kuuza mazao yao katika msimu mpya wa mavuno baada ya Serikali kuuagiza wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuanza kununua mazao hayo mapema iwezekanavyo.

Uamuzi huo wa Serikali, kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya uchumi na kilimo, utasaidia kuleta bei nzuri kwa wakulima na kuongeza usalama wa chakula.

Mei 23 Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aliigiza NFRA kuanza kununua mazao hayo kwa kuwa baadhi ya mikoa ikiwemo ya Rukwa na Katavi wameanza kuvuna mazao ya awali.

Katika uamuzi huo, Bashe aliwaeleza wanahabari jijini Dodoma Serikali inataka pia kulinda thamani ya mazao hayo.

Kwa mujibu wa Bashe Serikali imepanga kununua tani 100,000 za mazao ya chakula ambayo kwa kiwango kikubwa huwa ni mpunga na mahindi. Mazao hayo hutumika zaidi na Watanzania kwa chakula hasa katika kupikia ugali na wali.

Ujenzi wa vihenge vikubwa vya kuhifadhia mazao kama hiki kilichojengwa mkoani Rukwa utasaidia Serikali kuhifadhi kiwango kikubwa cha mazao kitachosaidia Taifa kukabiliana na njaa inapotokea .Picha|Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa.

Bashe amesema kuwa NFRA imekuwa ikinunua mazao kuanzia Juni na Julai jambo linalowanufaisha zaidi wafanyabiashara kuliko wakulima katika maeneo yenye misimu ya awali ya mavuno kati ya Aprili na Mei.

“Nimewaagiza NFRA…kuanzia kesho wanatakiwa kufungua vituo vya kununua mazao, kwa maana ya wiki hii, wanatakiwa kufungua vituo vya kununua mahindi na mazao mengine, katika mikoa ambayo uvunaji wa awali umeanza,” amesema Bashe.

Bei bado kigugumizi, wakulima waonywa

Licha ya msimu wa manunuzi kuanza Mei 24, 2022, Bashe hakuweka wazi bei rasmi itakayotumiwa na NFRA kununua mazao hayo kwa wakulima mwaka huu badala yake aliwataka maaafisa wa wakala huo kutoa wastani wa bei kulingana na ushindani wa soko katika eneo husika.

“Mwaka jana tulinunua kwa wastani wa Sh500 kwa kilo mwaka huu hatutanunua chini ya hiyo,” Bashe alisema huku akibainisha kuwa bei hizo hazitamuumiza mkulima.

Pamoja na Serikali kujipanga kuanza kununua mazao hayo, Bashe amewataka wakulima kutouza hazina zao zote badala yake wahifadhi kiasi kwa ajili ya chakula.

Wadau wa kilimo wanasemaje

Uamuzi huo wa Serikali umepokelewa kwa hisia mseto na baadhi ya wakulima wa Tanzania huku baadhi wakipongeza uamuzi huo na wengine wakionyesha wasiwasi kuwa huenda bei isiendane na gharama za kilimo.

Mbushi Kwilasa, mkulima wa mahindi Iringa vijijini ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) uamuzi wa Serikali kununua mazao yao mapema ni mzuri kuwa wafanyabiashara hununua kwa bei ya chini zaidi.

“Mwaka jana (2021) walinunua tani 100,000 lakini mwaka huu walipaswa kuongeza kwa kuwa NFRA wanapomaliza kununua mazao baadhi ya wafanyabishara hununua mazao kwa bei ya chini zaidi hivyo naiomba Serikali kuongeza kiwango cha kununua,” amesema Mbushi.

Kuna faida lukuki

Mtaalamu wa kilimo biashara kutoka Chuo cha Kilimo Sokoine SUA, Jery Masanja amesema wakulima wanaweza kunufaika zaidi kutokana na kuanza mapema kwa msimu wa manunuzi kwa kuwa kwa sasa NFRA itanunua mazao kwa kuzingatia bei ya ushindani iliyopo kwenye soko na gharama zilizotumika wakati wa uzalishaji.

“Kuna faida mbili ambazo zinapatikana, kwanza kama nchi tunapata uhakika wa chakula kwa sababu mazao haya yakinunuliwa yanaenda kuhifadhiwa, pili NFRA atapanga bNei kwa kuzingatia gharama zilizotumika wakati wa uzalishaji na ushindani wa bei ya zao husika,” amesema Masanja.

Pamoja na msimu wa manunuzi kuanza mapema, Aganyila Kamihanda, Ofisa wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kutoka Iringa anasema ununuzi huwa unapaswa kufanywa kwa umakini ili kuzuia kununua mazao ambayo hayajakauka vema na kusababisha unyevu nyevu unaozalisha sumukuvu ambayo huathiri mazao na afya za binadamu.

“Kwa kawaida msimu huanza mwezi Julai kwa kuwa mazao haya yakishanunuliwa huhifadhiwa kabla hayajaelekezwa kwenye matumizi mengine, sasa huwa tunanunua Julai ili kuyapa nafasi ya kukauka vizuri kwa kuwa yasipokauka hutengeneza sumu kuvu ambayo ni hatari kwenye mazao,” Kamihanda ameiambia Nukta Habari kwa njia ya simu.

Tanzania imeendelea kuwa tegemeo katika uzalishaji wa mazao ya chakula hususan mahindi na mchele kwa ukanda wa Afrika ya Mashariki.

Katika kipindi cha miaka mitatu (Mwaka 2019 hadi 2021), takwimu za Wizara ya Kilimo zinabainisha kuwa Tanzania imepeleka wastani wa tani 83,087 kwa mwaka katika nchi za ukanda huo sawa na asilimia 70 ya mahindi yote yanayouzwa nje ya nchi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live