Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali inakusudia kuimarisha mazingira ya biashara kwa kufanya mapitio ya kanuni za maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ya mwaka 2019 ikiwemo mtaji, ili kurekebisha masharti yaliyopo sasa na kupanua wigo wa utoaji wa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni.
Pamoja na masuala mengine, mapitio hayo yanatarajia kuanzisha madaraja ya maduka hayo kulingana na kiwango cha mtaji ambacho kinaweza kukidhi maeneo yenye wateja wengi na wachache.
Mapitio hayo pia yanalenga kuweka utaratibu utakaowezesha hoteli za kitalii nchini kutoa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni kwa wateja wao, ili kuongeza wigo wa utoaji wa huduma hii na hivyo kuchangia kutatua changamoto ya soko lisilo rasmi la kubadilisha fedha za kigeni nchini (black-market).