Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kukuza viwanda vya ndani madini

Madini Pic Data Serikali kukuza viwanda vya ndani madini

Fri, 8 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Madini, Dk Dotto Biteko, amesema serikali inaendelea kuhakikisha inafikia azma ya kusitisha usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi kupitia uimarishaji wa viwanda vya ndani vya kusafishia madini ghafi.

Dk. Biteko amesema hayo akiwa ziarani mkoani Geita, alipotembelea na kukagua kiwanda cha Kusafishia Madini ya Dhahabu kilichopo mjini Geita (GGR), ambacho kimejengwa na mwekezaji mzawa.

Amesema huo ni mwendelezo wa serikali kukuza sekta ya madini na kwa sasa inaendelea kuimarisha viwanda vya ndani vya kusafishia madini vilivyopo, ili madini ya dhahabu yaanze kuongezewa thamani ndani ya nchi.

“Kama mnavyofahamu serikali ya awamu ya sita imeweka nguvu kubwa sana kwenye uongezaji thamani ya madini na madini haya yanaongezwa thamani, ili yaweze kupata bei nzuri zaidi kuliko vile yangeweza kuuzwa nje ya nchi.

“Duniani hapa kuna nchi ambazo pengine hazina hata hayo madini ya dhahabu lakini vina viwanda kama hivi, sasa ni muhimu tuwe na viwanda vya namna hii ili kwanza ajira zibaki ndani na kodi nyingine zibaki hapa ndani.”

Ameeleza katika kuimarisha viwanda vya ndani vya madini, serikali imeshusha gharama ya tozo ya mirabaha ya dhahabu kutoka asilimia sita mpaka asilimia nne kwa dhahabu inayosafishwa kwenye viwanda vya ndani.

“Wito wangu kwa wachimbaji wote na wafanyabiashara wa madini, waone fahari kuona dhahabu ya Tanzani inasafishwa Tanzania, na inauzwa kwenye masoko ya nje ikiwa bidhaa ambayo tayari imekwishasafishwa,” amesema.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha GGR, Sarah Masasi amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kusafisha takribani Kg. 600 kwa siku kwa kiwango cha kimataifa na wanaendelea kuboresha miundombinu kutoa huduma kimataifa zaidi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live