Mwanza. Huku uamuzi wa kufungua masoko rasmi ya madini ukionyesha mauzo yameanza kuongezeka, Serikali imetangaza kuwashughulikia watu watakaojaribu kuyatorosha nchini ikisema licha ya kufungwa jela, watakuwa maskini kwa mali zao kufilisiwa.
Kwa mujibu wa katibu mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, masoko 17 yameshafunguliwa katika maeneo ya Geita, Kahama, Shinyanga, Namanga mkoani Arusha, Singida, Chunya, Ruvuma, Katavi, Dodoma, Kigoma, Tabora, Mara, Kagera, Mbeya, Mwanza, Iringa na Songwe.
Mpaka mwishoni mwa mwezi huu, masoko mengine yatakuwa yamefunguliwa Tanga, Mbulu na Babati mkoani Manyara, Kilimanjaro, Morogoro, Handeni, Lindi, Simiyu na Rukwa.
Akizindua Soko la Kimataifa la Madini mkoani Mwanza, Waziri wa Madini, Dotto Biteko alisema juzi kuwa, “nawatahadharisha wachimbaji na wafanyabiashara waache kutorosha madini nje ya nchi kwa sababu kufanya hivyo ni kujiweka kwenye hatari ya kugeuka maskini kwa mali zao kutaifishwa pamoja na kufungwa jela.”
Akizungumza mbele ya wafanyabiashara wadogo, kati na wakubwa wa madini, viongozi wa dini na watendaji wa Serikali, Biteko alisema Serikali itaendelea kutumia sheria, kanuni na taratibu kuziba mianya yote iliyokuwa ikitumiwa na watu wasio waaminifu kutoroshea madini nje ya nchi na kuikosesha Taifa mapato. “Hatutarudia makosa yaliyosababisha baadhi ya mataifa kujizolea sifa ya kuongoza kwenye soko la dunia kwa kuuza madini yanayopatikana Tanzania pekee.”
Machi 28, akizungumza na wanahabari jijini Mwanza, mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga alisema Serikali imetaifisha kilo 343 za dhahabu katika matukio tofauti yaliyohusiana na uvunjifu wa sheria kati ya Aprili, 2018 hadi sasa.
Pia Soma
- Mikakati yaanza Kigoma kuwa kitovu cha biashara Maziwa Makuu
- Mkojo wa sungura sasa lulu
- Mwongozo kuratibu ubunifu wanafunzi
- Mvua zinavyoitesa Dar, barabara zafungwa
Pamoja na kupongeza uamuzi wa kufungua masoko rasmi, mfanyabiashara wa madini mkoani Mwanza, Makona Kaniki aliiomba Serikali kuhakikisha yanakuwa na watumishi wa kutosha kulingana na mahitaji ili kuwaondolea wafanyabiashara adha ya kutumia muda mrefu kupata huduma.