Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kujipanga zaidi kuongeza pato la madini

C76cd90fa8eac0172e173f53ad4932a4 Serikali kujipanga zaidi kuongeza pato la madini

Fri, 23 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwenye sekta ya madini ili kuvutia uwekezaji wa ubia kati yake na wawekezaji wakubwa wa madini duniani.

Aliyasema hayo jana wakati akilihutubia Bunge jijini Dodoma. Samia alisema katika miaka mitano iliyopita, mafanikio ya sekta ya madini yamekuwa makubwa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mchango wake kwenye pato la taifa kutoka asilimia 3.4 mwaka 2015 hadi asilimia 5.2 mwaka 2019.

Alisema mapato kutoka sekta ya madini yameongezeka kutoka Sh bilioni 168 mwaka 2015 hadi Sh bilioni 527 mwaka 2020.

Rais Samia alisema serikali itaiwezesha sekta ya madini ikuze mchango na kufikia asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.

“Sekta ya madini ambayo kwa sasa imetoa ajira milioni 1.5 ina nafasi kubwa katika kuchochea ukuaji wa uchumi nchini. Kwenye miaka mitano iliyopita tumepata mafanikio makubwa kwenye sekta hii. Mwaka 2019 sekta ya madini imeongoza kwa kuliingizia taifa fedha nyingi za kigeni kiasi cha Dola za Marekani bilioni 2.7,”alisema Rais Samia.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita inakusudia kuendeleza mafanikio hayo kwa kusimamia Sheria ya Madini ya Mwaka 2017, kuziba mianya ya utoroshaji wa madini, na kuondoa vikwazo vya uwekezaji katika sekta hiyo.

Rais Samia alisema serikali pia itaimarisha masoko na minada ya madini, itahamasisha ujenzi wa viwanda vya uchenjuaji, uyeyushaji, usafishaji na utengenezaji wa bidhaa za madini kuweka mkazo kwenye matumizi ya teknolojia bora viwandani, kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kuwapatia mafunzo, mikopo na vifaa.

Alisema Shirika la Taifa la Madini (Stamico) litaimarishwa ili lishiriki katika shughuli za madini ndani na nje ya nchi.

Kuhusu nishati Rais Samia alisema katika miaka mitano iliyopita kulikuwa na mafanikio kwa kuongeza uzalishaji wa umeme hadi kufikia megawati 1,602 na kwamba mahitaji ya juu ya umeme nchini ni megawati 1,200.

Alisema serikali pia ilifanikiwa kufikisha umeme kwenye vijiji 10,294 sawa na asilimia 83.3 ya vijiji 12,317 vilivyopo.

“Pia tumeanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 ambao kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 43. Hivyo basi, Serikali ya Awamu ya Sita tutaendeleza jitihada za kuimarisha upatikanaji wa nishati nchini ikiwemo kukamilisha ujenzi wa Bwawa la Nyerere na kufikisha umeme kwenye vijiji 1,974 vilivyobakia,”alisema Rais Samia.

Alisema serikali imejipanga kuanza utekelezaji wa miradi ya kuzalisha umeme wa maji katika maeneo ya Ruhuji utakaozalisha megawati 358, Rumakali megawati 222, Kikonge megawati 300 na umeme wa gesi asilia Mtwara megawati 13, Somangafungu Megawati 330, Kinyerezi III megawati 600, na Kinyerezi IV megawati 300.

Alisema kutokana na mabadiliko ya tabianchi, kuna haja ya kuchanganya vyanzo vya nishati ili kuwa na uhakika wakati wote.

Alisema mazungumzo ya mradi wa gesi asilia (LNG) yamefikia miaka 6 sasa tangu yaanze, hivyo Serikali ya Awamu ya Sita itahakikisha inamaliza mazungumzo hayo ili mradi uanze.

“Tutafanya hivyo kwa kuwa vyanzo hivi ni endelevu na tunatarajia katika miaka hii mitano kuzalisha megawati 1,100 kupitia vyanzo hivyo. Tutaendeleza miradi ya kujenga njia za kusafirisha umeme kutoka Bwawa la Nyerere hadi kituo kikuu Chalinze na njia katika maeneo ambayo hayajaunganishwa na gridi ya taifa ili kupunguza gharama za uzalishaji umeme wa mafuta na kuokoa asilimia ya umeme inayopotea.”alisema Rais Samia.

Chanzo: www.habarileo.co.tz