Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma ya kuunganishiwa gesi asilia kwenye magari, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeanza mchakato wa kuongeza vituo vingine vya kutolea huduma hiyo ili kukabiliana na uhitaji.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Biashara ya Mafuta na Gesi kutoka TPDC Dkt. Wellington Hudson amesema, hivi karibuni kumekuwa na misururu mirefu ya magari kuingia kwenye vituo vya kujazia gesi baada ya kuwepo kwa idadi kubwa ya watumiaji huku kituo kimoja kikisitisha kutoa huduma kutokana na matengenezo.
Kuhusu mpango wa kuongeza vituo vingine mkoani Dar es Salaam Hudson amesema, TPDC itajenga vituo vingine 9 vya kujaza gesi kwenye magari, kazi itakayokamilika ndani ya kipindi cha miezi 24 kuanzia sasa.