Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kujenga mazingira mazuri biashara ya majani ya chai-Bashe

8727ba574c1a06a55f7e0494c2df91c8.jpeg Serikali kujenga mazingira mazuri biashara ya majani ya chai-Bashe

Sun, 18 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imesema juhudi zinafanyika kuhakikisha kwamba yanajengwa mazingira mazuri ya biashara ya majani ya chai nchini.

Mazingira hayo ni pamoja na kuhakikisha taifa linakuwa na mnada wa chai, sambamba na uanzishwaji wa maabara pamoja na maghala ya kuhifadhi chai hiyo .

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Kilimo, Hussein Bashe juzi wakati alipokutana na wadau wa sekta ndogo ya zao la chai kutoka serikalini na

sekta binafsi kwa lengo la kupata mrejesho wa hatua za uanzishwaji wa mnada wa zao la chai nchini.

Alisema mnada huo una manufaa makubwa kwa wakulima na taifa kwa ujumla.

Bashe akifafanua zaidi kuhusu kikao hicho alisema, lengo lilikuwa ni kujadiliana namna ya kuongeza uharaka wa juhudi za uanzishwaji wa mnada huo.

Kikao hicho kimewakutanisha Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai, Nicholous Mahuya, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Wakulima Wadogo wa Chai, Theophord Ndunguru na Mtendaji Mkuu wa

Soko la Bidhaa za Mazao ya Kilimo (TMX), Godfrey Malekano.

Wadau wengine wa sekta binafsi ni pamoja na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi, Angelina Ngalula, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa zao la Chai (TRIT) Dk Emmanuel Simbua, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya AGRI – CONNECT, Colin Scott na wasafirishaji wa mizigo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Bashe alisema katika kikao hicho kuwa serikali inafanya juhudi kubwa kuanzisha mnada wa chai nchini, kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi kwenye

sekta ndogo ya chai.

Aliongeza kwamba kwa kuwa na mnada nchini gharama za usafirishaji pia zitapungua na kutolea mfano kwamba usafirishaji wa kontena moja la majani ya chai la urefu wa futi ishirini kutoka Mufindi kwenda kwenye mnada wa Mombasa nchini Kenya, gharama yake ni shilingi milioni sita wakati kontena hilo hilo, likisafirishwa kutoka Mufindi kwenda, Dar es Salaam gharama yake ni Sh 3,000,000 .

“Tukipunguza gharama za biashara moja kwa moja na bei kwa mkulima nayo itapanda. Faida ya pili ya kuwa na mnada nchini ni

kuwa tutakuwa na uwezo wa kutawala (Control) bei ya chai sokoni na kuongeza uwazi wa mnyumbuliko wa gharama za uzalishaji wa chai kwa wakulima wetu,” alisema.

Pia alisema kwamba kwa kuwa na mnada Tanzania itakuwa na uhakika wa ubora wa madaraja ya chai kwenye soko kwa sababu kutakuwepo na maabara.

“Sasa hivi hatuna uwezo huo kwa kuwa udhibiti wa madaraja ya chai yetu, unafanywa na waendeshaji wa minada kwenye nchini nyingine,” alisema.

Bashe aliongeza kwa muda mrefu chai ya Tanzania imekuwa bora na

kusisitiza kuwa uanzishwaji wa maabara ya chai hapa nchini, utaongeza ubora wa chai maradufu kwa kuwa itakuwa rahisi kuitambua chai kwa ubora wake kijiografia.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Angelina Ngalula alisema sekta binafsi imejiandaa kushirikiana na serikali katika kujenga mazingira mazuri mazuri ya ufanyaji biashara ya majani ya chai.

Aidha alisema kuwa TPSF ipo tayari kununua vifaa vya maabara ya kisasa ya zao la chai pamoja na ujenzi wa majengo maalumu kwa ajili ya maabara hiyo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz