Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kujenga masoko manne

Acfea888113695dc3e925998ad49def4 Serikali kujenga masoko manne

Tue, 19 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema serikali itajenga masoko manne kwa kutumia fedha zake baada ya sekta binafsi waliokabidhiwa kazi hiyo kushindwa kutekeleza kwa mujibu wa makubaliano.

Makubaliano hayo yaliyofikiwa awali yalihusu pia soko la Mombasa ambalo sasa litajengwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF).

Pia wajasiriamali wametakiwa kujitokeza kuchangamkia Sh bilioni 31 zilizotengwa kwa ajili ya kuwainua kiuchumi.

Dk Mwinyi alisema hayo wakati alipofanya ziara ya kukagua miradi ya fedha za Covid-19 ambazo ni fedha za mkopo zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Dk Mwinyi alisema soko la Mombasa litajengwa kwa kutumia fedha za ZSSF, wakati masoko mengine tayari serikali imejipanga kutumia fedha zake na kuyajenga katika kipindi kifupi likiwemo soko la Mwanakwerekwe pamoja na Chuwini Unguja.

“Ujenzi wa masoko manne umezorota kwa sababu tumezipa kampuni binafsi kujenga na wameshindwa kutekeleza kazi hiyo kwa wakati... Nataka nisema kwamba ujenzi wa masoko hayo sasa utafanywa kwa kutumia fedha za serikali katika kipindi kifupi,” alisema.

Dk Mwinyi pia aliwataka wajasiriamali katika sekta mbalimbali kujitokeza na kuzichangamkia fedha zilizotengwa za Sh bilioni 31 kwa ajili ya kujiimarisha kiuchumi na kuondokana na umasikini.

Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mabanda ya wajasiriamali wa kusarifu bidhaa za mbao huko Karakana Chumbuni Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, alisema fedha za wajasiriamali zipo na walengwa wanatakiwa kujitokeza kuzichangamkia.

Dk Mwinyi amesema amefurahishwa na kazi nzuri inayofanywa na vikosi vya ulinzi ikiwemo JKU katika kujenga na kutekeleza miradi muhimu inayotumia fedha za Covid-19 ikiwemo ujenzi wa madarasa ya shule katika mikoa ya Unguja na Pemba.

Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhamed Mussa aliipongeza Serikali kwa kutenga Sh bilioni 68 katika sekta ya elimu ambapo fedha hizo zimelenga ujenzi wa shule za ghorofa tano pamoja na ukarabati mkubwa wa shule za zamani za mijini na vijijini Unguja na Pemba pamoja na ujenzi wa vyoo vya shule vipatavyo 1,680.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live