Mtwara. Serikali imesema tangu itangaze kubangua korosho zote nchini mpaka leo ni Shirika la kuhudumia viwanda vidogo (Sido) Mtwara kupitia wabanguaji wadogo ndio linaendelea na ubanguaji wa korosho ambapo tayari walishachukua tani 29.
Aidha Serikali kupitia bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko itatiliana saini mikataba na wamiliki wa viwanda vya ubanguaji Alhamisi Januari 10, 2019 kuanza ubanguaji.
Hayo yameelezwa leo Jumanne, Januari 8,2019 na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusema tarehe hiyo wataingia mkataba na wabanguaji wenye viwanda walioonyesha nia ya kuzibangua.
“Tutashuhudia mikataba ya kwanza ambayo bodi yetu ya nafaka na mazao mchanganyiko itakuwa inaingia mikataba na wenye viwanda kwa ajili ya kubangua. Kwa hiyo keshokutwa (Alhamisi) mikataba kati ya mitatu au minne ambayo imeshakamilika tutaingia nao mkataba hapahapa Mtwara,” amesema Hasunga.
Kuhusu suala la uhakiki wa wakulima wakubwa ili waweze kulipwa, matokeo hayaridhishi na kupelekea kelele kuwa nyingi kwani majina 9,075 yaliyotumwa katika mikoa husika kwa kushirikiana na kamati za ulinzi wilaya ili kuhakiki mashamba yao ni majina 521 pekee yaliyorudi huku majina 8,476 bado hayajarudishwa.
“Mkoa wa Mtwara tumepeleka majina 5,115 waliorudishwa kwamba wameshahakikiwa kwa malipo ni 93 tu, majina 5,422 majibu hayajarudi, Lindi tumepeleka 3,104 ambao mashamba yao wamethibitisha mashamba yao ni 428, lakini 2,598 bado majibu hayajarudi,”amesema Hasunga.
“Mkoa wa Ruvuma tumepeleka majina 365 hakuna hata jina moja limerudi, mkoa wa Pwani tumepeleka watu 91 hakuna majibu yaliyorudi. Sasa tumejaribu kufuatilia tumeona changamoto zilikuwepo, kwanza mikoa mingi hawakuwa na bajeti ya uhakiki hivyo usafiri ni shida,” amesema Hasunga.
Amesema changamoto nyingine mashamba hayajapimwa wala hayana alama hivyo shamba moja linaweza kuonyeshwa na watu watatu lakini pia vyama vya msingi havina daftari la majina ya wakulima.
“Wakulima wameuza unamwambia tuone daftari la wanachama hawana, kwa hiyo uhakiki unakuwa mgumu kwa sababu tulitegemea kama daftari la wanachama lingekuwepo ingekuwa ni sehemu ya kuanzia.”
“Huyu ni mwanachama analima wapi, anazalisha kiasi gani taarifa zingekuwepo kusingekuwepo na haja ya kwenda kuona mashamba,” amesema Hasunga
Kuhusu malipo amesema hadi kufikia jana Jumatatu Januari 7,2019 fedha zilizohakikiwa na zinatakiwa kuingizwa kwenye akaunti za wakulima ni Sh257.6 bilioni na fedha ambazo zilishaingizwa katika akaunti za wakulima ni Sh226.2 bilioni huku zaidi ya Sh30.7 bilioni zilizohakikiwa hazijaingizwa kwa akaunti kutokana na taarifa za wakulima kutofautiana.