Waziri wa Ujenzi na Usafi rishaji Profesa Makame Mbarawa amesema serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) ili kuwavutia wadau mbalimbali waweze kusafi risha mizigo yao kutoka Bandari za Tanzania kwa kutumia reli hiyo.
Aliyasema hayo jana baada ya kuzindua safari ya treni ya shirika hilo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kuelekea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kusafirisha kontena 20 zenye shehena ya mizigo ya Mpango wa Chakula Duniani (WFP) inayopelekwa katika kambi za wakimbizi.
Alisema kwa WFP kuiamini TRC na kuamua kushirikiana nao ni mafanikio kwa taifa kwani mpango huo unahitaji huduma ya viwango vya kimataifa hivyo TRC wamekidhi viwango hivyo na kuongeza kuwa WFP wameilipa TRC ili kusafirisha mzigo huo wa chakula hadi nchini DRC.
“Nawashukuru WFP kwa sababu wamekuwa wadau wetu wazuri, usafiri wa treni unapunguza gharama kwa asilimia 40, kama serikali tutafanya tunaloweza tutaweka miundombinu wezeshi ili wadau hawa WFP na wadau wengine zaidi waweze kuitumia reli yetu vizuri na kwa ufanisi zaidi,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa alisema ushirikiano kati ya WFP na TRC katika shughuli za uchukuzi ni muhimu sana kwa Tanzania kwa kuwa shirika hilo linashirikiana na kampyni au taasisi inayoweza kuwapa huduma za hali ya juu.
Alisema ushirikiano huo ni ishara kuwa ujio wa Reli ya Kisasa (SGR) utakuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania kwa kuwa wadau wengi wamevutiwa na huduma za TRC na kuamua kushirikiana nao katika kusafirisha mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda nje ya nchi.
Mkuu wa Kitengo cha Logistiki na Usambazaji wa WFP nchini Tanzania Mahamud Mabuyu alisema shirika hilo limekuwa mdau mkubwa wa TRC na litaendelea kushirikiana katika kuyafikia malengo yake hususani katika kupitisha mizigo yake.