Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kuifungua Kigoma kiuchumi

Afc9aa7eb9966a1ca904716d1e2eb749.jpeg Philip Mpango, Makamu wa Rais

Mon, 25 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema Serikali ya Awamu ya Sita itakamilisha ujenzi wa Barabara ya Uvinza – Malagarasi ili kufungua zaidi fursa za kiuchumi katika Mkoa wa Kigoma.

Alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Uvinza akiwa njiani kutoka Kigoma kwenda Dodoma.

Alisema serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo na kupitia ziara alioifanya hivi karibuni Dubai (Umoja wa Falme za Kiarabu), Mfuko wa Maendeleo wa Abudhabi uliiridhia kutoa fedha za ujenzi wa barabara hiyo.

Dk Mpango aliwataka viongozi katika ngazi za kata, wilaya na mkoa kusikiliza kero za wananchi na kuwashirikisha katika mipango ya maendeleo.

Aliuagiza uongozi wa Mkoa wa Kigoma kufika Wilaya ya Uvinza ili kukubaliana na wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi ikiwamo ya soko na stendi.

Aliwaahidi wananchi kuwa viongozi wa Wizara ya Maji na Wizara ya Nishati watafika wilayani Uvinza ili kutatua changamoto za maji na umeme ambazo zimetajwa kama kero za muda mrefu wilayani humo.

Awali, wananchi wa Uvinza walimueleza Makamu wa Rais changamoto zinazowakabili ukiwamo upungufu wa watumishi katika sekta za afya na elimu na mradi wa maji uliogharimu bilioni 1.7 hautoi huduma hiyo.

Wakati huohuo, Mkuu wa Wilaya Kigoma, Ester Mahawe ataongoza viongozi na wananchi wa wilaya hiyo kutoa zawadi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi aliyofanya kusimamia maendeleo ya wananchi.

Zawadi hiyo kwa Rais Samia itatolewa kwenye tamasha la kumpongeza litakalofanyika Aprili 27, mwaka huu kwenye viwanja vya Mwanga Community Centre mjini Kigoma.

Mahawe jana aliwaeleza waandishi wa habari mjini Kigoma kuwa, halmashauri mbili zilizopo katika wilaya hiyo zitaungana kufanya tamasha hilo.

Alisema moja ya mafanikio na kazi zilizofanywa na Rais Samia ni kuiwezesha wilaya hiyo kupitia halmashauri zake kupokea Sh bilioni 66.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwamo inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Mahawe aliitaja baadhi ya miradi iliyopata fedha kuwa ni ya afya, elimu, barabara na maji.

Alitaja moja ya maeneo yaliyopata mafanikio ni elimu ambapo bilioni 2.8 zilipokelewa kwenye halmashauri mbili za wilaya hiyo na kujenga madarasa 144 na kuwezesha wanafunzi 7,000 kupata sehemu za kusomea.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live