Serikali imepanga kugawa madume 336 ya ng’ombe yenye thamani ya Sh milioni 950 ambayo yatatolewa kwenye halmashauri 10 za wilaya nchini ili kuboresha sekta ya ufugaji.
Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaeleza kuwa sekta ya mifugo ni miongoni mwa sekta muhimu katika ukuaji wa uchumi.
“Kutokana na umuhimu huo, ni dhahiri kuwa ipo haja ya kuendelea kuimarisha ufugaji wa kisasa na kuchakata/kusarifu bidhaa za mifugo kwa ajili ya mahitaji ya ndani, ikiwemo ya lishe bora na usafirishaji nje,” imeeleza ilani hiyo.
Akizungumza wilayani Maswa mkoani Simiyu, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema kwa upande wa Wilaya ya Maswa, wafugaji wamewezeshwa madume 50 ya ng’ombe aina ya borani.
Ugawaji wa madume hayo umefanyika ili kuboresha sekta ya ufugaji kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kufanya mageuzi katika sekta hiyo.