Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kufuatilia uchunguzi wizi mil. 400/- za wateja NBC

Fedha Ed Serikali kufuatilia uchunguzi wizi mil. 400/- za wateja NBC

Sat, 10 Apr 2021 Chanzo: ippmedia.com

Ahadi hiyo ilitolewa jana baada ya Mbunge wa Jang’ombe (CCM), Ali Hassan Omar King, kuuliza swali la nyongeza bungeni na kuhoji lini wateja hao watalipwa fedha zao na kuichukulia hatua benki hiyo kwa kutowalipa.

 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Yusuph Masauni, alisema atafuatilia wizi huo ili kujua kama uchunguzi wa jambo hilo umefanyika na nani aliyesababisha uhalifu huo.

Alisema kama linasababishwa na mfumo wa kibenki basi Benki Kuu ya Tanzania (BoT) itachukua dhamana kuhakikisha fedha hizo zinarudishwa na benki husika.

Katika swali la msingi, Mbunge huyo alihoji wizi unapotokea kwenye akaunti ya benki ya mteja uliofanywa na mtumishi wa benki, ni nani mwenye wajibu wa kumlipa mteja.

Naibu Waziri Masauni alisema wizi unapotokea, uchunguzi wa kina hufanywa na vyombo husika katika masuala ya upelelezi ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kadri hali na mazingira ya tukio yatakavyokuwa.

“Endapo itabainika kuwa wizi huo umefanywa na mtumishi wa benki, hatua stahiki huchukuliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo ikiwa ni pamoja na mteja kulipwa kiasi alichoibiwa na mhalifu kuchukuliwa hatua za kinidhamu pamoja na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema.

Pia alisema BoT hutoa adhabu kwa benki husika pale inapobainika utaratibu uliowekwa na benki husika ulikuwa na kasoro zilizochangia kuibiwa kwa fedha za mteja.

Chanzo: ippmedia.com