Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kuendeleza wabunifu

Ustaarab Mmoja wa wabunifu wa teknolojia nchini

Mon, 9 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali kupitia COSTECH imesema haina lengo la kuwazuia wabunifu wadogo na kuficha kazi zao za kibunifu badala yake wanahakikisha usalama wa watu watakaotumia bunifu hizo.

Aidha, imesema itaendelea kuwatambua na kuwaendeleza wabunifu ambao wamejiajiri ili kutengeneza bidhaa za kurahisisha maisha ya watu.

Akizungumza jana Dar es Salaam katika kongamano la waandishi wa habari kuhusu Wiki ya Ubunifu Tanzania 2022, Mkurugenzi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk Amos Nungu amesema ubunifu umesaidia katika kutekeleza Mpango wa III wa maendeleo nchini na kwamba utasaidia vijana wengi kujiajiri.

Wiki ya ubunifu imeandaliwa na Mradi wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia mradi wa Funguo kwa kushirikiana na COSTECH, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na wadau wa sekta ya mawasiliano.

‘’Jukumu la serikali ni kulinda usalama wa watu wake. Kumekuwa na malalamiko mengi kuwa vijana wadogo wabunifu wamezuiwa kuendeleza kazi zao si kweli, kwa mfano kuna kijana kule Mbeya ambaye alibuni helikopta nilifika nikaiona lakini ni lazima tujihakikishie usalama wa abiria kama inaweza kuruka kulingana na viwango vya kimataifa na abiria watakuwa salama,’’ amesema Dk. Nungu.

Amesema kuwa wabunifu wamefanikiwa kujiajiri na kuajiri watu wengine kwa kuuza bunifu zao na kuliingizia taifa fedha ambazo zinachangia katika ukuaji wa uchumi.

‘’Kutakuwa na Wiki ya Ubunifu ambayo itaanza Mei 16 hadi 20, mwaka huu katika Mikoa 16 ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar, Mbeya na Morogoro ili kuona kazi za kibunifu zilizofanywa na vijana wetu zitakazosaidia kutatua changamoto katika jamii,’’ amesisitiza.

Kwa upande wake Mtaalamu wa Miradi wa UNDP, Emmanuel Nnko amesema kuwa ubunifu ni nyenzo muhimu katika kusukuma maendeleo katika nyanja mbalimbali.

Amefafanua kuwa ulimwengu wa sasa umebadilika hivyo changamoto zilizopo haziwezi kutatuliwa kwa kutumia mbinu za zamani badala yake kwa njia ya ubunifu.

"Lengo letu ni kuweka jukwaa la wabunifu ili kuonesha bunifu zao zilizoleta utatuzi katika changamoto mbalimbali katika jamii ikiwemo sekta za maji, elimu, mazingira, fedha, kilimo, uvuvi na utalii," amesema Nnko.

Pia amesema kuwa wabunifu wanatumia bunifu zao kuhakikisha zinaleta ufanisi na kuchagiza maendeleo endelevu na kwamba wapo wabunifu wengi mikoani ambao wanabuni vitu ambavyo vinajibu changamoto katika maeneo yao kwa kutumia teknolojia za kawaida.

"Tulipokea maombi zaidi ya 200 ambayo tulipata washindi 10 ambao tutawasaidia kukuza bunifu zao. Miongoni mwao ni waliobuni tochi kwa ajili ya kufukuza tembo na viboko wanaoharibu mazao shambani na waliobuni atamizi za kuangulia vifaranga kwa kutumia maganda ya mawese," amesema.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya mitaji, UNCDF, Paul Damocha amesema watahakikisha wanaendelea kuwafadhili wabunifu kupata fedha na huduma za kitaalamu ili kuendeleza bunifu zao.

Amesema kuwa mfuko huo kwa kushirikiana na serikali wamekuwa wakitengeneza miongozo mbalimbali ya kuwasaidia wabunifu kuja na bunifu zitakazotoa majibu ya matatizo yaliyopo katika jamii na kuthibiti kazi hizo ili ziweze kuwa na manufaa.

‘’Tutahakikisha wabunifu wote ambao bunifu zao zimetambuliwa na serikali wanapatiwa fedha na msaada wa kitaalamu ili kukubuni vitu vingi zaidi na kuajiri watu wengine,’’ amesema Damocha.

Hata hivyo wadau mbalimbali kwenye kikao hicho wametoa maoni na michango mbalimbali kwa COSTECH na Serikali katika kuhakikisha wabuni wanaendelezwa ili kuhakikisha ubunifu wao unakuwa na tija kwa Taifa la Tanzania ambapo baadhi yao wameeleza kuna wabunifu wengi wanaibuka lakini mwisho wa siku hawasikiki.

Wadau wengine wamesema pamoja na wabunifu kubuni mambo mbalimbali lakini wamekuwa wakikosa msaada wa Serikali na hivyo kubakia na ubunifu ambao hamnufaishi yeye wala nchi, hivyo wakiishauri serikali kuangalia namna nzuri zaidi ya kuhakikisha bunifu ambazo zinagunduliwa basi zinakuwa na matikeo chanya ikiwemo kuendeleza na kisha kutafutiwa masomo ya kuuza bunifu hizo.

Hata hivyo maoni hayo ya wadau yametolewa ufafanuzi mzuri na Dk.Nungu wa COSTECH ambaye alielezea namna ambavo wamekuwa wakiwasaidia wabunifu ila changamoto inayoonekana ni kutokuwepo kwa taarifa za mara kwa mara kuhusu wanavyoendeleza wabunifu hao ikiwa pamoja na kuwapatia mitaji na maeneo ya kuendeleza bunifu zao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live