Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kuendeleza hamasa kwa wakulima

Limaa Ed Serikali kuendeleza hamasa kwa wakulima

Mon, 12 Jul 2021 Chanzo: ippmedia.com

Hayo yalisemwa na Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda, wakati wa mazungumzo na Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Misaada la Kimataifa la Marekani (USAID), Andy Karas.
Katika mazungumzo hayo Prof. Mkenda alimweleza Mkurugenzi huyo kuwa Wizara ya Kilimo imejipanga kufanya mageuzi makubwa katika sekta hiyo ili kuondokana na dhana ya kilimo cha kujikimu na kuhamia katika kilimo cha kibiashara.

Waziri Mkenda, alisema kuwa ili kuongeza tija katika kilimo, serikali imejipanga kuimarisha utafiti katika mazao mbalimbali ya kibiashara na chakula.

Hata hivyo, alisema kuwa maendeleo ya kilimo yanategemea zaidi utafiti hususani wa udongo ili kujua kila eneo linapaswa kulimwa zao gani ili waweze kusonga mbele.


Alisema wizara imebaini teknolojia bora itakayopelekea kukisogeza kilimo katika hatua kubwa ya mafanikio na kimageuzi ili kuleta tija kwa wakulima.

Alisema pamoja na mambo mengine wizara pia imejipanga katika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kuliko kusafirisha bila kuongeza thamani.

“Tukiongeza thamani ni wazi kuwa uchumi utapanda, lakini zaidi ajira zitaongezeka kwa wananchi, tutakuwa na pato zuri la kigeni sambamba na utambulisho wa nchi,” alisema Prof. Mkenda.

Kuhusu sekta ya umwagiliaji Waziri Mkenda alisema Tanzania ina jumla ya hekta zaidi ya milioni 29, zinazofaa katika umwagiliaji, lakini ni hekta zisizofikia milioni moja ndizo ambazo zimefanyiwa kazi.

“Kwa maana hiyo kuna fursa kubwa katika umwagiliaji, hivyo ninyi kama wadau kadhalika natoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kuwekeza katika umwagiliaji,” alisema Prof. Mkenda.

Karas aliipongeza serikali kwa mikakati madhubuti ya kuimarisha sekta ya kilimo.

Chanzo: ippmedia.com