Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kuendelea kusaka masoko ya  mazao ya kilimo

7db099dbc73985721fa6d980a4b35828 Serikali kuendelea kusaka masoko ya  mazao ya kilimo

Sat, 13 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WIZARA ya Kilimo inaendelea kuwatafutia wananchi wake masoko ya ya mazao ya kilimo mbalimbali ikiwemo kununua mahindi na maharage kutoka kwa wananchi kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula na Bodi ya Mazao Mchanganyiko.

Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Josephine Gezabuke (CCM) ambaye alihoji, serikali ina mpango gani wa kutafuta soko la uhakika la mazao ya mahindi, maharage na muhogo.

Bashe alisema serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kutafutia wakulima masoko ya mazao ya kilimo ikiwemo kununua mahindi na maharage pia inafanya makubaliano ya kibiashara kati ya nchi na nchi, masoko ya kikanda, na kuwatafutia wakulima na wafanyabiashara masoko nje ya nchi kupitia balozi zetu.

“Aidha, serikali imeendelea kutoa vibali vya kusafirisha mazao nje ya nchi kwa njia ya mtandao (ATMIS), pamoja na kuacha mipaka wazi kwa ajili ya kuruhusu biashara ya mazao ya kilimo nje ya nchi. Imeendelea kutoa vibali vya kusafirisha mazao nje ya nchi bila ya masharti,” alisema.

Katika kipindi cha 2019/2020, serikali iliuza tani 111,846.69 za mahindi katika nchi za Afrika Mashariki na Kati ambapo Kenya walinunua tani 69,871.04, Uganda tani 19,081, Zambia tani 987.54, Rwanda tani 13,498.00, Burundi tani 7,253 na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo(DRC) tani 1156.11.

Katika kipindi cha Mei hadi Desemba 2020, Wakala wa wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula walinunua tani 73,831.147 za mahindi kutoka kwa wakulima na vikundi vya wakulima. Pia inaendelea kujenga ghala kwa ajili ya kuongeza uwezo wa kuhifadhi kutoka tani 251,000 hadi tani 501,000.

Bashe alisema Bodi ya Mazao Mchanganyiko imenunua tani 24,829.17 za mahindi kutoka kwa wakulima na vikundi vya wakulima. Aidha, wizara imeomba kibali kutoka Hazina kwa ajili ya kununua mahindi kutoka kwa wakulima.

“Serikali inaendelea kuwaunganisha wakulima na soko la maharage, katika kipindi cha Aprili hadi Desemba 2020, Bodi ya Mazao Mchanganyiko imenunua tani 1,743 za maharage kutoka kwa wakulima,” alisema.

Aidha, bei ya maharage imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, wastani wa bei kwa mfululizo wa miaka mitano kwa kipindi cha mwezi Desemba imeongezeka kwa asilimia 12. Wizara inaendelea kuhimiza wakulima kulima kilimo chenye tija kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo, alisema.

Wizara imeendelea kuhamasisha ununuzi wa muhogo na kuwa kampuni nne za Dar Canton, Jielong Holdings, TAEPZ na EPOCH Agricultural Development Company zimenunua tani 300 za muhogo mkavu kutoka kwa wakulima na inaendelea kutoa elimu ya kanuni bora za kilimo cha muhogo ili kupata bidhaa bora itakayokidhi mahitaji ya soko.

Chanzo: habarileo.co.tz