Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kuchunguza mwenendo wa ununuzi wa korosho msimu uliopita.

84757 Korosho+pic Serikali kuchunguza mwenendo wa ununuzi wa korosho msimu uliopita.

Mon, 18 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Serikali ya Tanzania imeunda timu ya watu watano watakaoshirikiana na  Kamati inayoshughulikia ununuzi wa korosho kuchunguza mwenendo mzima wa ununuzi wake kwa msimu ulipita baada ya kubaini udanganyifu katika baadhi ya maeneo.

Akizungumza leo Jumapili Novemba 17 2019, Jijini Dodoma, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema; “Tumeona kabla hatujamaliza kulipa na kufunga msimu, ni vema tujiridhishe katika mambo mbalimbali. Kilo zote zilizopokelewa katika vyama vyote, kama upungufu upo ni wa tani ngapi? Ni nani aliyesababisha ili tuweze kuchukua hatua zinazostahili.”

Amesema watahakiki majina yanayotoka katika vyama vya husika na kupelekwa katika mchakato wa malipo ili kujua kama kuna uchakachuaji.

“Tuhakiki kama kuna wakulima bado hawajalipwa. Maana mimi nimepokea simu nyingi tu za wakulima wakidai kutolipwa. Serikali imeshatangaza kuwa imemaliza malipo yote. Kama kuna wakulima hawajalipwa ni nani ambao hawajalipwa?” amehoji Waziri huyo.

Amesema pia watachunguza ni wakulima gani hawajalipwa na kwa nini.

Waziri Hasunga amesema kuna maeneo wamebaini walipwaji wamezidishiwa kilo kwa makusudi na kwamba, njama hizo zinadaiwa kufanywa na baadhi ya viongozi wao.

“Kwa sababu fedha zimetolewa na Serikali lazima tujiridhishe kuwa zimewafikia wakulima. Kwa hiyo tumeunda kamati ya watu wasiozidi watano ili washirikiane na kamati ya Wizara kuhakiki kiasi cha korosho kilichopokelewa, fedha iliyopatikana na kama kuna upungufu tubaini na ituhakikishie kuwa hao wakulima na wanastahili,” amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz