Serikali imesema itaboresha mfumo wa utoaji wa mbolea ya ruzuku kwa kuweka vifaa vya kusajili wakulima vya kutosha na kuongeza vituo vya kuuzia mbolea ili ipatikane mwaka mzima kwa wakulima vijijini.
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ameyasema hayo leo Alhamisi Januari 05, 2023 wilayani Mbozi mkoani Songwe wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili kuwa tayari uzoefu umepatikana mwaka huu kutoa mbolea ya ruzuku kupitia mfumo, lakini ili ufanye vizuri zaidi utaboreshwa zaidi katika msimu ujao.
Amesema miongoni mwa changamoto zilizotokea ni pamoja na wakulima kukaa muda mrefu kwenye foleni bila kupata huduma, matatizo ya kimtandao ambapo katika msimu ujao Serikali itaweka mfumo mzuri ikiwa ni pamoja na kuongeza vituo vya kutolea huduma 1,200 na kuvisajili viwe vingi zaidi.
“Kuanzia mwezi Julai mwaka huu vituo vyote vitakavyosajiliwa lazima vitakuwa na mbolea aina zote Ili mkulima mara tu anapovuna mazao yake akitaka kuuza mazao yake auze na anunue mbolea zote kwa ajili ya msimu unaofuata wa kilimo" amesema Bashe
Pia, Waziri Bashe amewataka mawakala kuongeza muda wa kuwahudumia wakulima badala ya kufunga maduka yao saa 9 kwa kuhofia usalama wao, amemtaka mkuu wa jeshi la polisi wilaya Mbozi kupeleka askali ili kulinda fedha za wafanyabiashara hao mpaka zitakapofika benki.
Kauli hiyo inafuatia kilio cha wakulima walitoa malalamiko kwa Waziri huyo kuwa wanakaa muda mrefu kwenye foleni na kupoteza muda mwingi huku wakiacha kazi nyingine za uzalishaji mali.
Feston Mwala ni mkulima toka kijiji cha Hasamba, amemweleza Waziri kuwa mfumo wa utoaji ruzuku uliotumika mwaka huu ni mzuri isipokuwa zipo changamoto chache ambazo ni ucheleweshaji na mbolea kutowafikia vijijini.