Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kuanza kununua mahindi kwa 500/- Agosti

89489f76795c46b52b5d073984367ee5 Serikali kuanza kununua mahindi kwa 500/- Agosti

Fri, 30 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imetangaza kuanza rasmi kununua mahindi kupitia Wakala wa Hifadhi ya Taifa(NFRA) mwezi ujao kwa bei ya Sh 500 kwa kilo moja katika mikoa yote inayolima zao hilo.

Hayo yalisemwa jana na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati akizungumza na wadau wa kilimo na viongozi wa ngazi mbalimbali wa wilaya ya Tunduru katika kikao kazi ambacho pia kilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Wilbert Ibuge.

Alisema serikali imeamua kununua mahindi kwa bei ya Sh 500 kwa kilo moja kutokana na wafanyabiashara kununua kwa Sh 250 ambayo hailingani na hali halisi ya uzalishaji hali ambayo inawaumiza wakulima.

“Hatua hii itasaidia sana kuwalinda wakulima ili kuwahi maandalizi ya msimu mpya wa kilimo 2021/2022,” alisema.

Bashe aliwapongeza viongozi wa serikali wilaya ya Tunduru wakiongozwa na mkuu wa wilaya hiyo, Julius Mtatiro kwa kazi nzuri wanayofanya kusimamia kilimo hususani cha korosho ambacho ndio kinaongoza kuipatia serikali mapato makubwa ya fedha za kigeni.

Alisema lengo la wizara yake ni kuona nchi inazalisha korosho tani 700,000 kwa mwaka.

Hata hivyo, alisema uzalishaji wa korosho unaendelea kuanguka kitakwimu, ambapo katika wilaya hiyo inayosifika kwa uzalishaji wa zao hilo nchini unaendelea kushuka mwaka hadi mwaka.

Kwa mujibu wa Bashe, katika wilaya ya Tunduru, uzalishaji umekuwa wa kusuasua, ambapo takwimu zinaonesha mwaka 2016/2017 ulikuwa tani 15,310, mwaka 2017/2018 ulikuwa tani 20,000, mwaka 2018/2019 tani 18,000 na mwaka 2020/2021 ulishuka zaidi hadi tani 14,000.

“Ni lazima wadau wa kilimo wakiwemo wakulima wajiulize tatizo la kuendelea kushuka kwa uzalishaji katika wilaya ya Tunduru linasababishwa na nini,” alisema.

Bashe alisema kwa upande wake, serikali imetafakari na kuamua kumuondolea mkulima mzigo wa pembejeo kwa kutoa pembejeo za ruzuku bure na mkazo mkubwa ni kupeleka dawa za maji badala ya za unga na zitafikishwa kwa kila chama cha msingi cha ushirika.

Alisema matarajio katika wilaya hiyo ni kupata dawa za maji lita 130,000 na tayari lita 48,000 za dawa aina ya salfa kilo milioni 2.7 zimeshafikishwa katika wilaya hiyo ambazo ni sawa na zaidi ya lita 900,000.

Alisema Wizara ya Kilimo itahakikisha dawa zilizobaki zitawafikia wakulima haraka.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Ibuge alisema mkoa huo wenye watu takribani milioni 1.6, uzalishaji wa chakula kwa mwaka 2019/2020 ulikuwa tani 787.321 wakati mahitaji yalikuwa tani 469,172, hivyo kuwa na ziada ya tani 318,149, mwaka huu uzalishaji ulikuwa tani 816,242 na hivyo kuwa na ziada ya tani 345,000.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro alisema wamekuwa wakikabiliwa na tembo wanaovamia mashamba na kuharibu mazao na ufugaji holela wa mifugo na kama changamoto hizo zisipopatiwa majibu haraka, uzalishaji katika wilaya hiyo utashuka kwa kiwango kikubwa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz