Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema kwa sasa Serikali inakamilisha kazi ya uandaaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ili kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati hiyo ifikapo Mwaka 2033.
Naibu Waziri Kapinga amesema hayo leo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Jacqueline Ngonyani Msongozi (Viti Maalum) aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuweka ruzuku kwenye Nishati ya Gesi ili Wananchi waweze kumudu na kutumia nishati hiyo.
Akijibu swali hilo, Mhe. Kapinga amesema “Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kutatua vikwazo vya matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza gharama za upatikanaji wake, vifaa na majiko sanifu ya kupikia.”
Ameeleza kuwa, Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia ni Ajenda ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na hilo lilitiliwa mkazo katika Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) uliofanyika Dubai, ambapo Rais, Dkt. Samia alizindua mkakati wa nishati safi ya kupikia kwa Wanawake Afrika. Hivyo, Wizara ya Nishati inalibeba suala la nishati safi ya kupikia kwa uzito mkubwa.
Kuhusu ruzuku katika mauzo ya mitungi ya gesi, Naibu Waziri amesema tayari kuna programu na miradi mbalimbali inayoendelea akitolea mfano programu ya ushirikiano na Umoja wa Ulaya (EU) ambapo Mawakala wanawezeshwa kifedha ili kupunguza bei ya mitungi ya gesi kwa watu wanaonunua mitungi hiyo kwa mara ya kwanza na kwamba Serikali itaendelea kubuni miradi na kutafuta fedha ili wananchi wapate gesi kwa gharama nafuu.
Ameongeza kuwa, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikibuni na kutekeleza Sera na Mikakati yenye lengo za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na utunzaji wa mazingira.