Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali imeunda timu ya kupitia upya mifumo ya mapato na kodi

Nchemba Ed Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba

Thu, 26 Aug 2021 Chanzo: ippmedia.com

SERIKALI imeunda timu ya wataalamu 10 watakaopitia mfumo wa ukusanyaji mapato na matumizi ya serikali, kupendekeza namna ya kuboresha kodi zinazotozwa ili kuweka mazingira wezeshi ya ufanyaji wa biashara hapa nchini.

Akizindua timu hiyo jana jijini Dar es Salaam yenye wajumbe wabobezi katika masuala ya uchumi, kodi, fedha na mifumo ya matumizi ya serikali, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema watakwenda kufanya tathmini na kutoa mapendekezo kwa serikali juu na namna bora ya ukusanyaji mapato kutakakoendana na ukuaji wa uchumi.

“Ni imani yangu kuwa timu hii ninayoizindua leo kwa miezi sita itakuja na mapendekezo yatakayoboresha mfumo uliopo pamoja na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na matumizi ya serikali, hivyo kuwa na bajeti endelevu,” alisema Dk. Nchemba.

Alisema sehemu ya majukumu mahsusi ya timu hiyo ni pamoja na kufanya tathmini ya mfumo wa kibajeti na kupendekeza namna bora ya kuiwezesha serikali kuwa na bajeti endelevu.

Jukumu lingine ni kufanya ulinganishi wa mfumo wa kodi wa Tanzania na nchi nyingine zinazofanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Dk. Mwigulu alitaja jukumu lingine ni kupitia ukusanyaji wa mapato na matumizi ya mifuko yenye vyanzo maalum na kushauri ipasavyo iwapo kuna haja ya kuendelea nayo au vinginevyo kwa lengo la kuboresha utekelezaji wa bajeti ya serikali.

Alitaja jukumu lingine ni kufanya tathmini ya mwenendo wa nakisi ya bajeti ya serikali na kutoa mapendekezo kwa kuzingatia mahitaji muhimu ya serikali.

Alisema timu hiyo itafanya tathmini ya ukuaji na ugharamiaji wa deni la serikali, ulipaji wa mishahara, ulipaji wa malimbikizo ya madai/madeni na ukuaji wake.

Kadhalika, alitaja jukumu lingine kuwa ni kupitia gharama, taratibu za uanzishaji na uendeshaji wa biashara nchini na kupendekeza namna ya kuboresha kodi zinazotozwa ili kuweka mazingira wezeshi ya ufanyaji wa biashara hapa nchini.

Dk. Nchemba alisema wastani wa ukusanyaji wa kodi katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ni asilimia 15.1 ya Pato la Taifa, wakati kwa nchi zilizoendelea zinakusanya hadi asilimia 40 ya pato la taifa au zaidi, kwamba kiwango hicho kinaziwezesha nchi zilizoendelea kugharamia kikamilifu matumizi muhimu ya kiuchumi na kijamii.

Alisema hata hivyo kiwango cha ukusanyaji wa mapato ya kodi nchini ni chini ya wastani wa ukusanyaji wa kodi katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Dk. Mwigulu alisema: “Kwa mfano mwaka 2020/21, jumla ya mapato ya ndani yalikuwa asilimia 13.3 ya pato la taifa, mapato ya kodi yalichangia asilimia 11.2 ya pato la taifa. Kiwango hiki kinadhihirisha kuwa Tanzania bado ina fursa ya kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato yanayotokana na kodi na yasiyo ya kodi ili kufikia walau wastani wa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Saraha.”

Chanzo: ippmedia.com