Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali imeongeza ufadhili wa utafiti kufanikisha viwanda

20360 Pic+ufadhili TanzaniaWeb

Tue, 2 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Uungwaji mkono wa Serikali kwa Shirika la Utafiti wa Viwanda Tanzania (Tirdo) umeongezeka kwa takriban asilimia 600 ndani ya miaka michache iliyopita hivyo kuchangia ongezeko la shughuli za utafiti nchini. Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo, Profesa Mkumbukwa Mtambo amezungumza na mwandishi wetu, Ludger Kasumuni na kubainisha mambo mengi.

Swali: unaweza ukatueleza historia fupi ya Tirdo?

Jibu: Tirdo ilianzishwa mwaka 1979, miaka miwili baada ya kufa kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), mwaka 1977. Wakati wa jumuiya hiyo, lilikuwapo shirika la utafiti la EAC ambalo makao makuu yake yalikuwa jijini Nairobi, Kenya.

Baada ya kuvunjika kwa jumuiya hiyo, Kenya ilikuwa ya kwanza kuanzisha shirika lake la utafiti (Kiri) kabla ya Tanzania na mwaka 2002 Uganda nayo ikafuata nyayo hizo kwa kuanzisha lake, (Uiri).

Swali: Ni kiasi gani cha ruzuku Tirdo hupokea kwenye bajeti ya kila mwaka kwa ajili ya kufanikisha utafiti?

Jibu: Sina kiwango halisi kichwani lakini nachoweza kusema nikwamba Serikali sasa hivi imeongeza mkazo na kujitoa kwake kumepanda kama mara sita hivi ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Mikataba na zabuni tunazopata zimeongezeka zaidi ya mara dufu.

Uungwaji mkono na Serikali umeongezeka kwa takriban asilimia 600, tunapata kazi nyingi za ushauri elekezi na mikataba ya kuanzisha viwanda vipya vya umma au kuboresha vilivyopo kuliko kipindi kingine chochote.

Serikali imetuamini kufanya utafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu kwenye miradi ya viwanda kwa asilimia 100.

Swali: Ni miradi au utafiti gani Tirdo imefanya miaka ya hivi karibuni?

Jibu: Ipo miradi mingi tuliyotekeleza na mingine bado inaendelea. Nitaitaja baadhi kwa uchache ambayo Serikali imetuamini na tukaisimamia. Tunashirikiana na Jeshi la Magereza pamoja na Shirika la Hifadhi ya Jamii (PSSF) kukiboresha kiwanda cha viatu kilichopo katika Gereza la Karanga mjini Moshi ili kuongeza uzalishaji wake.

Mpaka sasa, uwezo wa kiwanda hicho umeongezeka kutoka kuzalisha jozi 150 kwa siku mpaka jozi 450 na muda si mrefu kitazalisha jozi 500. Hii ni kwa sababu kuna shifti moja tu lakini zikiongezeka zikawa mbili, uzalishaji utafika jozi 800 kwa siku.

Dhamiri iliyopo ni kukiwezesha kiwand ahicho kuzalisha jozi 7,000 za viatu kwa mwezi pamoja na bidhaa nyigine za ngozi hivyo kukifanya kukifanya kuwa kikubwa zaidi ukanda wa Afrika Mashariki na kufikisha bidhaa 900,000 zilizokamilika kwa mwaka.

Tunashirikishwa kwenye baadhi ya miradi ya vyuo vikuu pia katika utoaji wa ushauri elekezi na utafiti katika jitihada za kuubadili uchumi wetu kuwa wa kati na unaotegemea viwanda.

Kwenye orodha hiyo kuna mkataba baina yetu na kampuni ya ushirika wa viwanda ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaa (Bicco) kujenga baadhi ya miradi mikubwa nchini.

Tunashirikiana na Chuo Kikuu cha Ardhi (Aru) kuchora, kupima na kuandaa maeneo ya viwanda. Kuna miradi tunatekeleza na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kutoa ushauri elekezi kwenye miradi ya kilimo mfano uanzishaji na ujenzi wa viwanda vya kusindika mazao.

Kuna mradi mkubwa wa utengenezaji wa chaki mkoani Simiyu unaoftumia gypsum kuzalisha chaki. Teknolojia hiyo ni matokeo ya utafiti tulioufanya.

Chaki zinazozalishwa hazitoi unga au vumbi kama wengine wanaliita hivyo ni rafiki wa mazingira. Kiwanda kimetoa ajira 5,000.

Kutokana na ufadhili wa Serikali unaoendelea, tunafanya upembuzi yakinifu na kuandaa mpango biashara kufanikisha ujenzi wa kiwanda cha kuchakata pamba kwa ajili ya bidhaa za matibabu hospitalini kama bendeji, POP, plasta (hogo) na pamba ya kusafishia na kufungia vidonda.

Mkoani Arusha, tunaandaa mpango na mchoro wa kiwanda cha viuatilifu huku tukiandaa mpango wa kujenga machinjio ya kisasa huko Sumbawanga.

Swali: Kuna nakisi yoyote ya bajeti unayoweza kuitaja kwa wakati huu?

Jibu: Sina namba kamili kwa sababu utafiti wowote duniani ni ghali. Hakuna kiwango maalumu kinachokubalika kwa ajili hiyo kwa kuwa gharama hubadilika kutokana na sababu kadhaa.

Swali: Mchango wa Tirdo serikalini na kwenye uchumi kwa ujumla?

Jibu: Nimeshakutajia kuhusu miradi na utafiti tuliofanya na tunaoendelea kufanya ambayo itatengeneza ajira nyingi haa kwa vijana licha ya kuokoa fedha za umma.

Kutokana na shughuli zetu, tunaokoa fedha nyingi za Serikali. Mchango wetu unazidi wa baadhi ya mashirika ya umma na wakala wa umma.

Swali: Ni maeneo gani ya kipaumbele mliyoyabainisha ili kuendana na msimamo wa sera ya sasa ya Serikali kujenga uchumi wa viwanda?

Jibu: Tunafanya kila tuwezalo kutekeleza sera ya viwanda ya nchi. Tunakusudia kuimarisha utafiti wetu hasa maeneo ya rasilimaliwatu, maendeleo ya teknolojia, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), maendeleo ya uhandisi wa vitu tofauti na uendelezaji wa teknolojia maalumu kwa mfano ya uchimbaji madini, viumbehai na uzalishaji wa bidhaa.

Swali: Tirdo inashirikiana vipi na mashirika mengine ya utafiti ndani na nje ya nchi?

Jibu: Tirdo ni mwanachama wa Jumuiya ya Mashirika ya Utafiti wa Viwanda (Waitro). Tunashirikiana na zaidi ya taasisi 2,000 nchini. Tunazikaribisha taasisi binafsi pia kushirikiana nasi.

Chanzo: mwananchi.co.tz