Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali ilivyowezesha biashara bucha za nyamapori

A284a3ae1ec53e6077ba5dde296b3eb3 Serikali ilivyowezesha biashara bucha za nyamapori

Mon, 28 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tangu mwaka 2020 serikali imetoa leseni 73 kuanzisha bucha za nyamapori katika mikoa ya Tanzania Bara.

Ofisa Mhifadhi Wanyamapori wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Gregory Kalokole alisema walipokea maombi 66 ya kufungua bucha hizo na baada ya ukaguzi mabucha 39 yalikidhi vigezo na kupewa idhini ya leseni katika mikoa 16.

Biashara ya bucha za nyamapori ilianzishwa kwa kuzingatia agizo la Serikali la Oktoba 10, 2019 kupitia kwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk John Magufuli.

Wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Katavi, Dk Magufuli alisema ni muhimu wananchi wafaidi rasilimali za nchi kwa kuwa na bucha za wanyamapori.

Baada ya agizo hilo, uandaaji na utayarishaji wa mwongozo uliandaliwa zikiwemo Kanuni ya Bucha iliyoanzishwa Februari 7 mwaka 2020 kupitia Tangazo la Serikali Namba 84 la mwaka 2020.

Kalokole alisema aina ya wanyamapori wanaoruhusiwa kuvunwa, aina ya ndege, bei zao na utaratibu wa kutoa leseni kwa wamiliki wa bucha umeainishwa kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 383 la Mwaka 2020.

Bucha ya kwanza ilifunguliwa Dodoma Desemba 20 mwaka 2020 na hadi mwaka jana leseni zilizotolewa kwa biashara hiyo zilikuwa 34.

Kalokole aliitaja mikoa iliyopewa idhini ya kupata leseni za bucha hizo kuwa ni Mwanza, Mbeya, Mara, Tabora, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Arusha, Shinyanga, Singida, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma na Katavi .

Alisema hadi sasa wamilikiwa wa bucha 73 wamepewa leseni 16 kati ya hizo zinafanya kazi.

Alizitaja bucha hizo na mikoa yao kuwa ni One Mile Ltd -Mikocheni(Dar es Salaam), Paul Maganga Nswima-Kinyerezi(Dar es Salaam), Shafi Transort Services-Magomeni Mikumi (Dar es Salaam) na Teste of the Wild Butchery eneo la Buza Temeke (Dar es Salaam).

Alizitaja bucha nyingine kuwa ni Kitegengi Enterprise, Chang’ombe mkoani Dodoma, Oscar Haule Kidulile mjini Ifakara na Mpango Mpangile Agrovet-Dakawa(Morogoro), Yero 2020 General Supply na Hosea Elia Hangali, zilizopo Babati,Sauti ya Walemavu-Mererani (Manyara).

Nyingine ni Ches Company Ltd -Mianzini na Pori Butcher-Kwa Morombo na Finyasi D Mafie Game Meat-Mtaa wa Sokoni (Arusha),Aron Kessy Chenda -DDC-Mbalizi(Mbeya),NBS Game Meat-Mihayo(Tabora) na Japhet Msuka Bangili Busega-Ramadi (Simiyu).

Alisema Tawa imeruhusu aina 18 za wanyamapori wawindwe. Alitaja bei za wanyama kuwa ni pamoja na pundamilia anayeuzwa Sh300, 000 kwa Watanzania na Sh 600,000 kwa wageni.

Nyati ni Sh 200,000 kwa Watanzania na Sh 400,000 kwa wageni, na pofu Sh 300,000 kwa Watanzania na Sh 600,000 kwa wageni.

Tohe – ndupe –dume Sh 100,000 kwa Watanzania na Sh 200,000 kwa wageni, Tohe – kusi-dume Sh 100,000 kwa Watanzania na Sh 200,000 kwa wageni, Kongoni/Konzi Sh 100, 000 kwa Watanzania na Sh 200,000 kwa wageni, Swala tomi-dume Sh 50,000 kwa Watanzania na Sh 100,000 kwa wageni.

Kuhusu utaratibu wa kutoa leseni, Kalokole alisema Kamishna wa Uhifadhi anatakiwa kukiri kupokea maombi kutoka kwa waombaji ndani ya siku 14 na kuyawasilisha kwa Kamati ya Ushauri ya Bucha za Nyamapori kwa uchambuzi kwa kuzingatia vigezo vilivyoinishwa kwenye kanuni za bucha za nyamapori.

Ndani ya siku 14 za kazi,Kamishna Uhifadhi atafanya uamuzi na kuwajulisha waombaji kwa barua kama maombi yao yamekubaliwa au yamekataliwa kwa kutoa sababu husika na kama atatoa cheti, kitatumika kwa miaka mitano.

Alisema Tawa haihusiki moja kwa moja kutoa bei elekezi kwa wamiliki wa bucha kwa kuzingatia gharama za kuwapata wanyamapori katika mazingira yao ya asili na vifaa vinavyotumika kuwindia.

Tozo ya usajili wa bucha Sh 250, 000 na tozo ya leseni ya kumiliki nyara Sh 50,000 kwa kila mwombaji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live