Rais Samia Suluhu Hassan Septemba 20, 2023 alihitimisha ziara yake ya kimkakati ya siku saba katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani.
Yafuatayo ni mambo mbalimbali yaliyofanyika wakati wa ziara hiyo kwenye sekta ya ujenzi na uchukuzi.
Katika sekta ya ujenzi na uchukuzi Rais Samia Suluhu Hassan alikagua maboresho yaliyofanyika katika uwanja wa ndege wa Mtwara ambapo mpaka sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 98.
Mradi huo umehusisha kupanua njia ya ndege kutua (Runway), ujenzi mpya wa matabaka ya barabara ya kurukia na kutua ndege, kuongeza urefu wa barabara ya kurukia na kutua ndege, kujenga maegesho mapya ya ndege, kujenga barabara mpya ya magari ya kuingia uwanjani pamoja na maegesho ya magari, usimikaji wa taa za kuongozea ndege, kujenga uzio wa usalama kuzunguka uwanja, kuweka mfumo wa umeme wa akiba na kuweka vifaa vya zimamoto na kujenga tenki la kuhifadhi maji na ununuzi wa gari la zimamoto.
Katika miradi ya barabara Rais Samia alifungua rasmi barabara ya Mtwara - Mnivata yenye urefu wa Kilomita 50 iliyojengwa kwa fedha za mapato ya ndani. Barabara hiyo imejengwa kwa kiwango cha lami katika eneo la Naliendele mkoani Mtwara ikiwa imegharimu shilingi Bilioni 93.8.
Kwa upande wa sekta ya Uchukuzi Rais Samia amekagua maboresho ya gati ya bandari ya Mtwara ambapo Serikali imeweka mikakati ya kuiendeleza bandari hiyo ili ifikie au kulingana na bandari ya Dar es Salaam.
Rais Samia Suluhu Hassan aliweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara ya Ruangwa - Nanganga yenye urefu wa kilomita 53.5 kwa kiwango cha lami katika kijiji cha Nandagala, mkoani Lindi.