Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, amesema ukaguzi wa maduka ya kubadilishia fedha za kigeni nchini umebaini uondoshwaji wa fedha katika mfumo rasmi na kutekelezwa kwenye utakatishaji wa fedha haramu.
Dk Mpango ametoa ufafanuzi huo leo Jumatatu Aprili mosi 2019 jijini Dodoma katika mkutano wake na waandishi wa habari, akiwa ameambatana na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga.
Amesema katika kazi hiyo iliyofanywa mikoa ya Arusha na Dar es Salaam imebaini pia upokeaji wa amana kutoka kwa wafanyabiashara kinyume cha matakwa ya leseni za biashara husika.
Mengine ni kudhoofisha thamani ya shilingi, pamoja na mambo mengine ambayo yalianza kuathiri usalama wa nchi.
"Kwa mfano maduka yaligundulika kutumia fedha nyingi za Tanzania kununua fedha za kigeni, lakini fedha ndogo za kigeni hazikuwa na taarifa ya fedha za kigeni zilizobaki," amesema.
Related Content
Amesema katika kazi hiyo hakuna fedha yoyote iliyotaifishwa na kwamba taratibu za kisheria zilifuatwa wakati wa kuchukua vielelezo mbalimbali.
Amevitaja vitu hivyo kuwa ni fedha, kompyuta, simu za viganjani, mashine maalumu za kuhifadhia taarifa na taarifa mbalimbali ili kusaidia uchunguzi.