Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali haitaki masihara bandari

2308da15669e2dc94232d5f34856780c.jpeg Serikali haitaki masihara bandari

Sun, 20 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imesema jicho lake liko kwenye Bandari ya Dar es Salaam kwa kuwa ni eneo muhimu kwa uchumi wa nchi na lango la biashara. Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara alisema jana kuwa sehemu kubwa ya mapato ya nchi yanapatikana kupitia bandari hiyo hivyo serikali haitaki masikhara.

Waitara alisema hayo jana alipofanya ziara kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) Dar es Salaam na kuzungumza na menejimenti ya mamlaka hiyo na Bandari ya Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo ambayo Waitara alihimiza huduma nzuri kwa wateja, alikemea uwepo wa makundi miongoni mwa wafanyakazi katika bandari na kusema yanaweza kuathiri ufanisi wa utoaji huduma.

Waitara alisema wateja wanapohudumiwa vizuri wanakuwa mabalozi wa kupeleka ujumbe kwa nchi jirani kuwa huduma katika Bandari ya Dar es Salaam ipo vizuri.

Aliwataka wafanyakazi wote kuanzia uongozi wa juu mpaka langoni kujua kwamba serikali na wananchi wanawategemea.

“Kila unapotoa huduma, ujue kwamba unatoa huduma kwa niaba ya Watanzania wengi wanaotazamia kazi yako iwe nzuri.

Mheshimiwa Rais Samia anaposema tunataka fedha safi na kodi ambayo siyo ya kushurutisha, kuhuzunisha na kufilisi watu, anamaanisha watu ambao mmesimama mahali ambapo kuna biashara, ifanyike biashara halali,”alisema Waitara.

Aliongeza, “Mtu ahudumiwe vizuri kwa maana ya kumjali mteja, ahudumiwe kwa wakati bila mizengwe ili akawaambie wenzake

kwamba ukitaka kupata huduma ya haraka nenda katika Bandari ya Dar es Salaam… usipobadilika utalazimishwa kubadilika kitu ambacho kinaweza kuathiri utendaji wako wa kazi kwa sababu mabadiliko yanaweza kuwa chanya au hasi.”

Akemea makundi Katika hatua nyingine, Waitara alikemea makundi miongoni mwa wafanyakazi akisema, ana taarifa wapo wanaojiita ‘Wenyeji wenye bandari yao’ na kundi linaloitwa ‘Wakuja’.

“Nawashauri hao wanaoitumia kauli hii, serikali hatutaki kusikia kwamba hapa kuna mtu wa kuja au mtu mwenye bandari yaani wa zamani.

Hata kama kuna mtu amekuja hapa ana mwezi mmoja au miwili na wewe mwingine una miaka 10 au 15, wote ni watumishi wa serikali, sisi tunachotaka ni ufanisi, habari kwamba huyu amekuja juzi, huyu sijui wa zamani, hii haipo,”alisema Waitara.

Aliendelea, “Mlikuwa na mtendaji mkuu, na mwenye mamlaka ya nchi akafanya mabadiliko kwa kumteua Erick Hamisi kuwa Mkurugenzi Mkuu hapa, mabadiliko haya huna uwezo wa kuhoji kwa sababu si mamlaka yako.

Matarajio ya Mkuu wa nchi ni kwamba tufanye maboresho na tufanye kazi, ndiyo maana nasisitiza lugha ya kwamba hapa kuna mtu wa kuja na mwenyeji isiwepo.”

Waitara alisema Mtendaji Mkuu wa TPA, Hamisi si mpya katika kazi kwa kuwa alikuwa katika Bandari ya Mwanza akifanya kazi hizo za bandari, hivyo wanachotakiwa ni kumpa ushirikiano kila mtu kwa nafasi yake na kwa uzoefu wake na siyo kumkwamisha.

“Mambo ya kukaa kwenye kijiwe na kujadili mara huyu amekuja juzi, huyu ameletwa tu hapa, tukikugundua kwamba na wewe unakwamisha, ukweli ni

kwamba nafasi yako itakuwa matatani na wewe mwenyewe utakuwa matatani, kwa sababu haya ni maelekezo ya serikali na Mheshimiwa Rais ameshafanya uamuzi,” alisema Waitara.

Waitara alisema ameambiwa kuna watu bandarini wanafanyakazi kwa maelekezo kutoka mtaani jambo alilosema ni baya. “Yaani kwamba kuna mtu alikuwa anafanya kazi hapa, nafasi yake sasa haipo, lakini wewe ili ufanye kazi kwa kutumwa na huyu aliyepo, lazima umpigie simu yule mjadiliane, akujaze upepo halafu uje hapa ufanye kazi chini ya kiwango, hiyo siyo sawasawa, toeni ushirikiano wa kutosha kwa mkurugenzi mkuu.”

Undugu pia alisema kuna tatizo la undugu kwenye bandari hiyo na aliwahi kumtuma mlinzi wa nafasi ya chini akampa taarifa za kushangaza licha ya kuwepo kwa vyombo vya serikali kila kona ya bandari hiyo.

Aliwataka watu wa vyombo vya ulinzi na usalama bandarini hapo kufanya kazi waliyopelekwa kuifanya waisaidie nchi vizuri kwa kuwa ikitokea serikali ikapata taarifa tofauti na za kwao, tafsiri yake ni kwamba wapo bandarini hapo kwa kazi nyingine.

Pia aliitaka TPA kushughulikia tatizo la tozo la nauli ya kivuko Buchosa Mwanza na Nyamisati Mafia ambako wananchi wanalipa Sh 1,200 kitu ambacho Rais Samia alishaagiza kifanyiwe kazi.

“Sehemu ya manunuzi kuna malalamiko mengi, panahitaji kufanyiwa maboresho, kuna malalamiko makubwa ya manunuzi yaliyokuwa yanafanyika ama kwa bahati mbaya au kwa makusudi, mtu unatengeneza nyaraka ambayo ina gharama kubwa kwa kuzingatia sheria, kwa hiyo unaweza kuiba kwa kutumia sheria na kuingizia serikali gharama kubwa,”alisema Waitara.

Chanzo: www.habarileo.co.tz