Katibu Mkuu wa wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amesema, Serikali itaendelea kuwalinda Wawekezaji wanaowekeza nchini.
Dkt. Abdallah ameyasema hayo mkoani Iringa alipokutana na kusikiliza changamoto za wamiliki wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za mazao ya misitu hususani Vinia inayotumika kutengeneza bidhaa mbalimbali.
Kwa upande wa wawekezaji, amewataka kuendelea kuwekeza kwa kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira bora na wezeshi pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara Nchini (MKUMBI).
Dkt. Abdallah amesema wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara itashirikiana na mkoa wa Iringa pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS ) kutatua changamoto zote zilizojitokeza ili wawekezaji hao waendelee kuzalisha bidhaa hizo kwa tija.
Naye Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Iringa, Asifiwe Mwakibete ametoa rai kwa Wawekezaji mkoani humo kuendelea kuwekeza katika viwanda vya mazao ya misitu kwa kuwa malighafi ya miti inapatikana kwa wingi, na kwa Wananchi amewataka waendelee kupanda miti kwa kuwa soko la miti ya mbao ni kubwa.