Dar es Salaam. Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya mafuta ya Total imesema itafanya utafiti wa mafuta nchini ili kuongeza kasi ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kwa kutegemea kiwango cha mafuta kitakachogunduliwa.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nishati Medard Kalemani wakati wa hafla ya kuwapongeza wafanyakazi na wadau wa kampuni hiyo ya mafuta katika maadhimisho ya miaka 50 ya kampuni hiyo hapa nchini inayoadhimishwa wiki nzima kwa shughuli mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Kalemani alisema kuwa tafiti zinaonyesha kila mahali ilipogunduliwa gesi asili chini yake kuna mafuta hivyo Serikali imeanza mazungumzo na kampuni hiyo ili kufanya utafiti wa mafuta nchini.
Hata hivyo Kalemani amewataka Watanzania kuionyesha ushirikiano kampuni hiyo ambayo alisema ni mshirika muhimu katika maendeleo ya nchi.
“Naipongeza kampuni hii kwa kazi inazozifanya nchini ikiwemo kuchangia maendeleo ya taifa, kutoa ajira za kudumu na za muda kwa Watanzania, kusambaza nishati mbadala ya jua, kuchangia huduma kwa jami pamoja na ujenzi wa bomba la mafuta la Uganda,” amesema Kalemani.
Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Total Tanzania, Tarik Moufaddal amesema katika kipindi cha miaka 50, kampuni ya Total imefanya makubwa kwa kutoa huduma mbalimbali kwa jamii kwa lengo la kuhakikisha taifa linasonga mbele.
Pia Soma
- Waziri atoa matumaini ya kuuza korosho
- Majaliwa kuteta na wanahisa wa CRDB Arusha
- Kipindi cha televisheni cha udaku chafutwa baada ya mgeni kufariki saa chache baada ya kuhojiwa