Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali: Mageuzi ya mashirika ya umma sio kushindana na sekta binafsi

SejtAAA.jpeg Serikali: Mageuzi ya mashirika ya umma sio kushindana na sekta binafsi

Mon, 11 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imesema mageuzi inayofanya kwenye mashirika ya umma yenye sura ya kufanya biashara hayamaanishi kuwa inataka kuleta ushindani kwa sekta binafsi.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dk Hashil Abdallah alipokuwa akitoa ufafanuzi na kusema lengo ni kuboresha utendaji wa taasisi hizo, ili kuboresha huduma na hivyo kukidhi mahitaji ya wateja na kupata faida inayoziwezesha kujiendesha zenyewe.

Ufafanuzi huo umetolewa kutokana na kuwepo wasiwasi ulioonyeshwa na baadhi ya wadau kuwa mageuzi hayo kwenye taasisi za umma huenda ni mwanzo wa Serikali kuingia kwenye biashara na kuleta ushindani kwa sekta binafsi.

Wachumi waliozungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili, Machi 10,2024 wamesema kuwa ni wazo zuri kwa mashirika ya umma kujiendesha yenyewe, lakini bei za gharama za huduma zao inatakiwa ziwe ndogo ili kujitofautisha na sekta binafsi, kwani jukumu la msingi la Serikali ni kutoa huduma kwa wananchi kwa gharama nafuu.

Lakini, Dk Abdallah amewatoa hofu kwa kusema Serikali haina mpango wa kuingia kwenye biashara kushindana na sekta binafsi na kwamba haitasahau jukumu lake la msingi la kuwapatia Watanzania huduma bora kwa gharama rafiki.

“Tunataka taasisi za umma zishindane kufikiri na kufanya shughuli zao kibiashara, ili zitoe huduma bora katika jamii na kupata faida itakayoziwezesha kujiendesha,” amesema Dk Abdallah.

Akizungumza hivi karibuni mkoani Arusha, Rais Samia Suluhu Hassan alisema Serikali haitavumilia mashirika ya umma ambayo yatakuwa yanajiendesha kwa hasara.

Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Abel Kinyondo amesema sekta za umma zikitoa huduma kwa bei nafuu, zitavutia wateja wengi na hivyo kupata faida kubwa.

Amesema hii itachagia taasisi hizo kujiendesha zenyewe na kutoa gawio kwa Serikali

“Taasisi za umma kujiendesha kibiashara itaipunguzia Serikali mzigo, kwani zitakuwa na uwezo wa kusimama zenyewe bila msaada kutoka serikalini,” amesema Profesa Kinyondo.

Lakini, ametoa angalizo kuwa ili hilo liwezekane, inapaswa huduma zinazotolewa ziwe na ubora mkubwa, zitolewe kwa wakati na kwa ulimi mtamu.

“Taasisi za umma zinapaswa kutoa huduma kwa bei nafuu ikilinganishwa na sekta binafsi. Kwa upande mwingine, taasisi hizo zinapaswa kuendesha shughuli zake kwa gharama ndogo ili zisipate hasara,” amesema Profesa Kinyondo.

Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Mwinuka Lutengano amesema kama mashirika ya umma yatajiendesha kama ya kibiashara yataweza kustawi vizuri.

“Kazi ya Serikali ni kutoa huduma, lakini ili taasisi ya umma ijiendeshe huwezi ukakwepa moja kwa moja ‘elements’ za biashara.

“Kama ilivyo kwa sekta binafsi, kwenye sekta za umma kunahitajika ufanisi, ubunifu na utoaji wa huduma bora kwa wakati,” amesema.

Ili kuwa na ufanisi mkubwa kwenye sekta za umma, Dk Lutengano ameonyesha haja ya kuwa na ubia na sekta binafsi pale inapobidi, jambo ambalo Serikali inasema iko tayari kufanya hivyo.

Kwa upande wake, mchumi na mtaalamu wa biashara Dk Donath Olomi, amesema licha ya kwamba taasisi za umma zina jukumu la kutoa huduma, zina nafasi ya kuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi kama zitafanyiwa mageuzi makubwa ya kiutendaji.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi za serikali, sekta ya umma inachangia asilimia 20 ya ajira zote nchini na chini ya asilimia moja kwenye pato la Taifa.

“Ili kuongeza mchango wa sekta ya umma kwenye uchumi wa nchi, mashirika ya umma yanapaswa kuwa na ubunifu na kutoa huduma bora kwa wakati,” ameshauri Dk Olomi.

Amesema ili mashirika hayo ya umma yafanye vizuri, lazima wanaopewa dhamana ya kuyaongoza wawe na fikra za kibiashara.

Dk Olomi ameongeza kuwa watakaoaminiwa kuongoza mashirika hayo wapimwe kwa matokeo.

“Lazima kuwe na utaratibu wa ufuatiliaji na uwajibikaji,” amesisitiza.

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu hivi karibuni alisema ili kuhakikisha mashirika ya umma yanasimama imara, ni lazima wakurugenzi, wenyeviti na wajumbe wa bodi kuwa na ujuzi wa sekta husika wanayofanya kazi.

“Tunataka (serikali) tufaidike na uwekezaji wetu wa Shilingi trilioni 70.67 kwenye mashirika ya umma,” alisema Mchechu.

Mpaka kufikia Aprili mwaka jana, kulikuwa na mashirika ya umma 298, ambapo 248 kati ya hayo Serikali ndio mwenye hisa nyingi zaidi. Tafsiri yake ni kwamba Serikali ina hisa chache kwenye mashirika 50 tu kati ya 298

Chanzo: www.tanzaniaweb.live