Serikali imewatoa hofu Watanzania na kuwataka kuwa wavumilivu kuhusu kupanda kwa bei ya vyakula, ikieleza kwamba hali iliyopo sasa ni ya mpito na bei itashuka.
Imesema imeshaweka mikakati ya kuhakikisha hali iliyopo sasa inaondoka na taifa halitarudi tena katika nyakati kama hizi.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, aliyasema hayo jana Ikulu jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan jijini Dakar, Senegal Januari 25 hadi 27 mwaka huu.
“Mimi ninaamini hii ni transition (mpito) na bei ya chakula itashuka. Tutaondoka kwenye taifa la kuwa tegemezi, kwamba kwa miaka minne ijayo taifa litakuwa katika nafasi nzuri.
“Ni ukweli bei ya vyakula imepanda lakini ni vizuri tukafahamu kwanza serikali hii iliingia madarakani ilikutana na matatizo makubwa manne, la kwanza ni ugonjwa wa corona, ambao uliathiri nchi katika usambazaji wa pembejeo, kwa maana ya kusafirisha nje na kuleta ndani.
"Pili, ni vita vya Ukraine na Russia, tatu ni mabadiliko ya tabianchi na nne ni kupanda kwa gharama za mafuta duniani,” alifafanua Bashe.
Alisema matatizo hayo ikiwamo vita vya Ukraine na Russia yameiathiri nchi kwa sababu Tanzania ni waagizaji wa bidhaa za kilimo, mbegu na mbolea kutoka nje.
Alifafanua kwamba chakula kinachotumika leo hakijazalishwa sasa bali kilizalishwa msimu wa mwaka 2021/22.
Alisema bei ya mbolea kwa mwaka 2020/21 ilikuwa ni wastani wa Dola za Marekani 300, lakini ulipoingia msimu wa kilimo wa mwaka 2021/22 ambao mavuno yake yalifanyika Juni mwaka jana, bei ya mbolea ilipanda kwa zaidi ya asilimia 200.
Bashe alisema mkulima aliyelima mpunga wilayani Mbarali mkoani Mbeya, mfuko wa mbolea ya kupandia ulipanda kutoka Sh. 50,000 hadi 140,000, mfuko wa mbolea ya kukuzia ulipanda kutoka Sh. 45,000 hadi 120,000, hivyo kusababisha gharama za uzalishaji kwa mkulima kuongezeka.
"Leo ukinunua mchele daraja la kwanza wilayani Nzega, ukienda mashineni utaununua kwa Sh. 2,500, hadi Sh. 2,700, ukiusafirisha kuja Dar es Salaam mwaka 2020 gharama ya kusafirisha kwa kilo moja ilikuwa Sh. 70, leo ni Sh. 210
“Hapo maana yake gharama ya mafuta imepanda, gharama za usafirishaji zimepanda. Sasa huyu mkulima wa Mbarali gharama za uzalishaji mwaka 2020 na msimu wa kilimo wa mwaka 2021/22 zilipanda kwa zaidi ya asilimia 200, sasa ni lazima gharama za chakula zitapanda," alisema Bashe.
HATUA ZILIZOCHUKULIWA
Bashe alisema Rais Samia alipoingia madarakani aliweka ruzuku katika mafuta, mbolea na mbegu.
Alisema: “Hali hiyo inamaanisha kwamba mkulima aliyenunua mbolea katika msimu wa mwaka 2021/22 kwenda shambani kuzalisha, aliyenunua kwa Sh. 140,000 kwa mfuko mmoja. Msimu wa kilimo 2022/23 ambao chakula chake tutakivuna kuanzia Aprili, Mei na Juni mkulima huyu alinunua mfuko wa mbolea kwa Sh. 70,000."
Alisema hatua ya pili, serikali imeweka mikakati ya muda mrefu ili tatizo lililotokea lisijirudie tena.
Bashe alisema Rais Samia anatarajia kuzindua kiwanda cha mbolea kitachozalisha metric tani milioni moja, wakati mahitaji ya mbolea kwa sasa nchini ni tani 400,000 hadi 600,000.
Alitaja mkakati mwingine ni serikali kuanza kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji na kuachana na kutegemea mvua, kwamba mabonde 22 yapo katika utafiti wa kuhakikisha maji yake yanatumika katika kilimo cha umwagiliaji na serikali imetenga Sh. bilioni 36 katika mchakato huo.
WANUNUZI KUTOKA NJE
Bashe pia alitoa ufafanuzi kuhusu wafanyabiashara kutoka nje kuja nchini na kununua mazao, akisema: "Mazao ya kilimo ni ya mkulima, ni mali yake na sio ya umma, wana haki ya kuyauza popote na kumuuzia mtu yeyote. Tutamruhusu mtu yeyote kutoka sehemu yoyote kwenda kununua mazao sehemu yoyote".
Bashe alisema endapo serikali ikihitaji kununua mazao itakwenda kununua kwa wakulima kwa bei elekezi ya soko.