Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sekta ya usafirishaji yachanja mbuga

Mabasi Sekta ya usafirishaji yachanja mbuga

Fri, 20 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imesema kumekuwa na ongezeko la utoaji leseni 284,158 za usafirishaji kwa mwaka huu ukilinganisha zilizotolewa mwaka jana, huku katika pikipiki za magurudumu mawili (Bodaboda), zikiwa zinaongoza.

Akizungumza jijini leo Dar es Salaam kwenye mkutano na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini ukiandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo amesema idadi ya leseni za usafirishaji zilitolewa mwaka jana ni 230,253.

“Katika mgawanyiko huo, pikipiki za magurudumu matatu (Bajaji) ni asilimia 24, malori asilimia 19, Teksi mtandao (Ride Hailing) 17, teksi Kawaida (Cab) asilimia 13, huku mabasi ya masafa marefu yakichukua asilimia sita (6),” amesema.

Amesema kukua huko kunaenda sambamba na ukusanyaji wa mapato ambapo katika kipindi hicho yameongezeka kutoka Sh25.9 bilioni za mwaka jana hadi Sh34 bilioni mwaka huu ikiwa asilimia 32 ya ongezeko, huku akidokeza kuwa: “Kutokana na mafanikio haya hadi mwakani tumejiwekea malengo ya kufikisha Sh40.1 bilioni.”

Amesema ndani ya kipindi hicho mapato yatokanayo na leseni yameongezeka kwa asilimia 41, Levi za watoa huduma asilimia 24 mapato mengine asilimia 14 huku yatokanayo na adhabu yakipungua.

“Mamlaka inaendelea kufanikiwa kujenga tabia ya utii wa sheria na kupunguza adhabu kwa watoa huduma za usafiri ardhini nchini,” amesema.

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu (3), mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2022/23, mamlaka imechangia Sh14 bilioni katika mfuko mkuu wa serikali.

“Kwetu ni mafanikio makubwa na kwa kipindi chote tangu kuanzishwa kwa ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) hatujawai kupata hati chafu,”amesema

Awali, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara, Johansen Kahatano, amesema mamlaka hiyo inaendelea kuboresha usafiri wa umma katika majiji na miji

“Katika jitihada za kulifungua jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine Tanzania Bara, tumeanzisha njia za daladala ili kufika maeneo yasiyofikika kwa urahisi na kwa gharama nafuu,” amesema

Ametolea mfano katika jiji la Dar es Salaam amesema njia saba mpya zimeongezwa ikiwemo ya kutoka Kivukoni kwenda Bunju Sokoni kupitia Barabara ya Bagamoyo na kutoka Gerezani kwenda Bunju Sokoni kupitia Barabara ya Bagamoyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live