Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Sheikh Shakhbout bin Nahyan Al Nahyan amesema Tanzania inayo nafasi kubwa ya kuendelea kupata wawekezaji hususan katika sekta ya kilimo, kutokana na mazao yanayolimwa nchini humo.
Waziri Nahyan ameyasema hayo jana Ijumaa Oktoba 30, 2021 alipotembelea banda la Tanzania kwenye maonyesho ya Expo 2020 yanayoendelea katika Jiji la Dubai.
Mbali ya kuwavutia wafanyabiashara wengi na wawekezaji, lakini maonyesho hayo pia yamekusanya maelfu ya watu kutoka mataifa mbalimbali duniani wanaoendelea kufika Jijini Dubai kwa lengo la kutembelea mabanda ya maonyesho ya nchi tofauti.
Mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Johanaspher Shapher amesema ili Tanzania ifanikiwe zaidi kwenye sekta ya kilimo, iwekeze zaidi katika sekta ya miundombinu kwa lengo pia la kuwavutia wawekezaji.
"Baba yangu ameishi sana Tanzania eneo la Mbozi (Mkoa wa Mbeya kabla ya sasa kuwa Songwe), alikuwa anasoma sana Kahawa, lakini tatizo ni barabara na mambo mengine, kwa hiyo Serikali itengeneze miundombinu rafiki itakayowavutia zaidi wawekezaji," amesema Shapher.
Wakati mdau huyo akishauri hayo, Waziri Al Nahyan amesema miongoni mwa mambo aliyovutiwa nayo ni kwenye sekta ya Kilimo.
"Ninapenda kufahamu zaidi aina mbalimbali ya mazao yanayolimwa kwa wingi Tanzania," amesema waziri huyo.
"Zao hili la parachichi nimevutiwa nalo sana," amesema.
Waziri Al Nahyan amesema "Lakini pia napenda kujua ni kiasi gani Tanzania imewekeza katika kilimo na uzalishaji wa maparachichi."
Ametoa rai kwa Serikali kuendelea kukitangaza kilimo cha zao hilo kusudi wawekezaji waweze kufahamu ili waanze kuwekeza nchini.
Wakati huo huo, waziri huyo ameipongeza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupata Rais wa Kwanza mwanamke, Samia Suluhu Hassan.
Amesema hiyo ni hatua kubwa ya kuelekea katika usawa wa kijinsia huku akisisitiza kuwa Tanzania iko kwenye mikono salama ya mama wa Taifa.
"Mko katika mikono salama ya mama. Mtaendelea kusonga mbele kiuchumi na kijamii," amesema waziri huyo.