Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sekta ya kilimo ni soko kubwa la Bima linaloogopwa nchini

9809 Kilimo+pic TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kampuni nyingi za bima nchini zinalitazama soko la bima ya kilimo au mazao kama ‘chuma cha moto’ kwamba yeyote atakayejaribu kukigusa atakiona cha mtema kuni.

Hofu yao kubwa ni kupata hasara kutona na sekta yenyewe kuhodhiwa na watu wenye kipato cha chini (wakulima wa jembe la mkono) ambao nao wamezingirwa na changamoto nyingi.

Kwanza, wengi wao hawakopesheki na taasisi nyingi za kifedha, suala la migogoro ya ardhi, changamoto ya sera za kilimo na kutotabirika kwa bei ya mazao.

Kwa mujibu wa mamlaka ya usimamizi wa bima nchini (Tira) kwa kipindi kirefu, kukosekana kwa takwimu za mazao na hali ya kilimo ambazo hutegemewa katika kufanya tathimini ya hatari iliyopo katika zao fulani, ndicho chanzo cha wakulima kutonufaika na huduma za bima.

Watoa huduma za bima wanasema kukosekana kwa takwimu na taarifa hizo za kilimo hapa nchini husababisha wao kushindwa kupanga namna ya kufanya biashara bila kupata hasara kwakuwa wanafahamu ukubwa wa hatari mapema.

Hata hivyo bima za aina hiyo zimekuwa ni hitaji kubwa la wakulima wote wakiwemo wadogo lakini wamekuwa hawapati fursa kama yalivyo matarajio yao.

Mussa Kabele ambaye amefanya kilimo kwa miaka 10 sasa anasema kuna changamoto kubwa ya hali ya hewa nchini hivyo uwepo wa bima utatoa ahueni ahueni kwa wakulima.

Kamishina wa bima nchini Baghayo Saqware anasema endapo kampuni zitajitoa kuhudumia kilimo zitakuwa zimeunga mkono juhudi za Serikali katika mpango wake wa kuwa na asilimia kubwa ya Watanzania wanao nufaika na huduma za bima lakini pia uchumi wa viwanda.

“Uchumi wa viwanda unahitaji sekta ya bima iliyo imara kwakuwa viwanda vingi vinavyoanzishwa vinahitaji huduma ya bima. Hivyo kila ubunifu unaofanywa na kampuni ya bima ili kukuza upatikanaji wa huduma hiyo hususani katika kilimo ambacho ndiyo uti wa mgongo, Tira tutamuunga mkono ,” anasema Saqware.

Anasema Suala la bima kwa wakulima ni hitaji la muda mrefu la Serikali na wakulima wenyewe mpaka kuna wakati Tira ilianza kuwashawishi wakulima kuanzisha bima yao wenyewe kwa kuzingatia mahitaji yao lakini hawakufanikiwa.

“Kama Serikali tunaendelea kuandaa mazingira ili kuhakikisha kampuni nyingi zaidi zinatoa huduma hiyo kwa sekta ambayo ni uti wa mgongo katika uchumi wa nchi.

“Sera ambayo inaonyesha majukumu ya kila wizara katika kuboresha sekta ya bima likiwamo suala la kuwa na takwimu za mazao, tayari imeandaliwa na sasa ipo kwa waziri wa fedha ambaye anaipitia kabla ya kuiwasilisha kwenye Baraza la Mawaziri kwaajili ya maboresho na hatua nyingine,” anasema Saqware.

Ofisa mipango na uwekezaji wa kampuni ya bima ya Zanzibar Insurance, Rahim Hamza anasema kila kampuni inahitaji faida katika biashara inayoifanya, hivyo wao watakuwa tayari kutoa huduma hiyo endapo sekta itawahakikishia kupata faida.

“Bima ya kilimo ni tatizo, kwasababu sekta yenyewe bado haijawa imara, kampuni yetu bado haijafikiria kuwa na bima ya aina hiyo labda mpaka pale kilimo cha umwagiliaji kitakapostawi. Ni vigumu leo hii mimi kumpa bima mtu aliyelima ekari mbili tu na hana uhakika wa maji wala mbolea,” anasema Hamza.

Wakati kampuni nyingine za bima zikiendelea kusubiri, Serikali iandae takwimu za kilimo na hali ya hewa ndipo zianze kutoa bima ya kilimo, kampuni ya bima ya Strategis Insurance ilitangaza kujitosa kuianza biashara hiyo.

Strategis ilikuwa ikizindua rasmi mpango wake wa kupanua wigo wa kibiashara kutoka huduma moja (bima ya afya) kuwa bima ya jumla (General insurance), ilitangaza kuwa miongoni mwa huduma zake itakuwa ni bima ya kilimo.

Ofisa Mkuu wa kampuni hiyo, Kain Mbaya anasema kwa sasa kampuni yake inakamilisha mifumo ya utoaji wa huduma za jumla na ndani ya miezi miwili, utakuwa umekamilika hivyo hata huduma za kilimo zitakuwa zikipatikana kwa urahisi katika kampuni yao.

“Kuna changamoto ya kutokuwapo kwa takwimu jumuishi kuhusu kilimo na mazao hapa nchini, lakini katika mpango wetu wa biashara, tutashirikiana na wizara ya fedha na wizara ya kilimo kwa wakati huu ambao tunasubiri kuimarishwa kwa takwimu hizo na nina imani tutafanya biashara,” anasema Mbaya.

Ofisa huyo anasema walengwa wakubwa katika biashara hiyo ni wakulima ambao wapo vijijini ambako kampuni hiyo haina matawi, lakini imejipanga kuwafikishia huduma kidijitali pale itakapobidi.

“Kwa sasa kampuni yetu ipo ndani ya kampuni 10 bora zilizoteka soko, tunataka mpango huu utufikishe kwenye tano bora,” anasema Mbaya.

Ofisa mkuu wa mipango na masoko wa Strategis, Emmanuel Jimmy anasema bima yao itahusisha wadudu kushambulia mazao, ukame, mafuriko, moto na wizi kabla ya zao husika kuvunwa, lakini pia kama litakosa soko.

“Kabla ya kupanga bei ya bima, kampuni itapima gharama za uendeshaji wa shamba na faida inayotarajiwa baada ya mavuno. Thamani ya shamba ndiyo itakayoamua kiasi ambacho mkulima anapaswa kulipia kama bima,” anasema Jimmy.

Aidha, endapo kampuni hiyo itafanikiwa kuanzisha bidhaa hiyo ya bima itaweka rekodi kwakuwa miongoni mwa kampuni chache zilizofanikiwa kutoa bima zipo ambazo zimejaribu kutoa bima ya mbegu lakini ufanisi wake haujawa na matokeo makubwa.

Ukiachilia mbali Strategis ambayo kwa sasa ipo kwenye mpango wa kampuni ya bima ya MGen imekuwa katika biashara hiyo tangu 2013 lakini imekuwa ikiwahudumia wakulima katika vikundi.

“Wateja wetu ni wakulima wakubwa na wakati ambao wapo kwenye makundi, kabla ya kuwajumuisha katika huduma, tunawapatia elimu ya kilimo na bima kwanza,” anasema Derrick Sebastian Msimamizi wa masoko wa kampuni hiyo.

Anasema mpaka sasa kampuni yao inayafikia makundi mapya 1,000 kila mwaka huku bei ya wastani ikiwa Sh25,000 kwa ekari moja.

Kuhusu bima nchini

Kasi ya ukuaji wa sekta ya bima nchini katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, imekuwa kwa asilimia saba lakini wananchi wa kipato cha chini hususani wa maeneo ya vijijini sio wanufaika wakubwa wa sekta hiyo muhimu.

Mpango uliopo sasa ni kuwa na asilimia 50 ya Watanzania watu wazima wanaotumia huduma za bima ifikapo 2028.

Kwa mujibu wa Tira, kuna kampuni za bima 31 nchini, madalali zaidi ya 150, mawakala zaidi ya 150 na wakadiria hasara zaidi ya 50.

Januari mosi mwaka huu, Tira iliidhinisha waraka wa masharti katika biashara namba 055/2017 kwaajili ya kusaka Sh300 bilioni ambazo zipo kwenye kampuni za bima za nje ya nchi zikitokea nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz