Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sekta binafsi zaitwa kuwekeza miundombinu ya usafirishaji Tanzania

Lami Barabaraaaa Sekta binafsi zaitwa kuwekeza miundombinu ya usafirishaji Tanzania

Mon, 12 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imezitaka sekta binafsi kuwekeza kwenye miundombinu ya usafirishaji ikiwemo barabara, reli na anga ili kukuza uchumi kupitia sekta hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Februari 11, 2024 jijini Dar es Salaam kwenye warsha iliyowakutanisha wadau wa sekta ya usafirishaji, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema tayari Serikali imeshawekeza katika sekta hizo, hivyo ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika ukuaji wake.

“Uwekezaji wote ambao Serikali imetekeleza umefanywa na sekta ya umma, hivyo katika mkutano huu nimewaambia wajadiliane namna sekta hizo zinaweza kushiriki kikamilifu kuwekeza kwenye uboreshaji wa miundombinu yetu ya usafiri.

Amesema kupitia mkutano huo ulioandaliwa na Tume ya Mipango, Serikali inategemea wadau hao watatoa taarifa na mapendekezo mazuri namna sekta binafsi zinaweza kushiriki kwenye uwekezaji.

Pia, Profesa Kitila amesema ni wakati muhimu kwa kuwa kwa sasa kinaelekea kipindi cha Bunge la Bajeti, ili mapendekezo hayo yaingie kwenye mpango wa maendeleo.

“Tuko katika hatua za kuandika dira mpya ya maendeleo, hivyo tunaamini wadau watatoa mchango mkubwa wa namna dira hiyo iseme kwenye upande wa sekta ya usafirishaji kuelekea mwaka 2050,” amesema.

Pia, amebainisha kuwa maendeleo ya miundombinu ndio kiashiria kikubwa cha maendeleo ya nchi yeyote ile.

Amesema nchi zilizo kwenye jiografia ya pwani na maji kama bahari, mito na maziwa ni rahisi zaidi kuendelea ukilinganisha na nchi zisizo kwenye jiografia ya namna hiyo.

Wakati Profesa Mkumbo akiyasema hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi, David Kafulila amesema wanataka kuhakikisha sehemu kubwa ya uchumi inajengwa na sekta binafsi.

Kafulila amesema wanataka kuona mchango wa sekta binafsi unakuza sehemu kubwa ya uchumi, kwa sasa uwekezaji mkubwa unafanywa na Serikali hivyo wanataka sekta hiyo itoe mchango wake.

"Hivyo sisi kama Kituo cha Ubia tuna kazi ya kuunganisha fursa zilizopo serikalini zichukuliwe na sekta binafsi waweze kuzitumia," amebainisha Kafulila.

Akitolea mfano barabara ya Kibaha, Chalinze hadi Morogoro amesema itakuwa ya kwanza kujengwa na kuendeshwa na kampuni binafsi, watu watakuwa wakilipia barabara hiyo, hivyo itarahisisha maendeleo.

"Tumezoea kuona barabara zinajengwa na kusimamiwa na Serikali, sasa hii itajengwa na sekta binafsi na tuko kwenye mchakato wa kupata kampuni hiyo," amesema.

Kadhalika, Kafulila amesema kwa mujibu wa mpango wa maendeleo ya miaka mitano ijayo, jumla ya Sh40.6 trilioni zinatarajiwa kutumika kwenye miradi ya maendeleo itakayoendeshwa na sekta binafsi.

Amesema hivyo utekelezaji wake unaanzia kwenye mikutano kama hiyo inayowakutanisha wadau ili waeleze changamoto walizonazo katika kutekeleza miradi hiyo ya ubia, ili Serikali iweze kuwarahisishialengo likiwa kuhakikisha ukuaji wa uchumi unajengwa na sekta binafsi.

Awali, mwekezaji sekta ya Utalii kutoka jijini Arusha, Wilbert Chambulo amesema kwa upande wa uchumi wa utalii miundombinu ni muhimu kwa kuwa watalii wanaitumia kufikia maeneo ya vivutio.

Chambulo amesema watalii wanategemea miundombinu kama maji, anga na barabara hivyo mapendekezo watakayoyatoa yataelekeza uboreshaji ambapo matokeo yake ni kupokea watalii wengi zaidi nchini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live