Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sekta binafsi yamlilia bilionea Ali Mufuruki

87835 TPSF+pic Sekta binafsi yamlilia bilionea Ali Mufuruki

Fri, 13 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi Binafsi Nchini Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye amesema kifo cha mfanyabiashara maarufu, Ali Mufuruku kimeacha pengo kwa tasnia ya sekta binafsi.

Amesema ni kiongozi aliyejitoa kuhakikisha sekta binafsi inapiga hatua.

Amesema Mufuruki alianzisha chama cha wakurugenzi wakubwa mabapo kwa sasa kina wanachama 110 ili kuhakikisha kuwa ndiyo sekta binafsi inasonga mbele kwa ajili ya kuendeleza jamii.

Simbeye ameyasema hayo leo alipowasili nyumbani kwa marehemu Mbezi beach jijini Dar es Salaam kuungana na watanzania kutoa pole kwa familia.

Mufuruki amefariki jana alfajiri katika hospitali ya Morningside jijini Johannesbarg nchini Afrika ya Kusini alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kutibiwa wiki moja katika Hospitali ya Aga Khan akisumbuliwa na homa ya mapafu.

“Sekta binafsi imepata pigo, marehemu ametuachia jukumu kubwa la kuyaendeleza yale aliyoyaanzisha enzi za uhai wake, tutamkumbuka kwa mchango wake katika sekta hii ambapo leo hii tunajivunia kuwa na sekta binafsi Tanzania,” amesema.

Amesema Mufuruki alijitolea kuboresha mazingira ya biashara kuwa wezeshi ili kuiingizia Serikali mapato.

“Alikuwa mpambanaji wa rushwa, alikuwa akisisitiza viongozi wote wa kampuni binafsi na Serikali kufanya kazi kwa maadili, mara nyingi alisisitiza kuwa rushwa ni adui wa haki kamwe tusiipe nafasi,” ameongeza Simbeye.

Naye Sadi Kajuno, jirani na rafiki wa Mufuruki amesema watamkumbuka kwa upendo wake na mawazo yake ambayo mara zote yalikuwa yakiwajenga.

“Tumempoteza rafiki mpenda dini na muda wote alikuwa akisisitiza kusaidia jamii, alikuwa msaada kwa majirani muda hakuwa mwenye majigambo licha ya kuwa mtu mwenye kipato cha juu alikuwa akipokea ushauri na mawazo yetu pia,” amesema Kajuno.

Chanzo: mwananchi.co.tz