Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

…Sekta binafsi kuboreshwa kupaisha uchumi

814c5311f2428a7bfe6eee096a006607 …Sekta binafsi kuboreshwa kupaisha uchumi

Tue, 8 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali itaendelea kushirikiana na wajasiriamali kujenga na kuiboresha sekta binafsi, itoe mchango wenye manufaa makubwa kwa taifa.

Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 imeielekeza serikali ihakikishe katika miaka mitano ijayo, watendaji wake wanaendelea kuwa na mtazamo kuhusu sekta binafsi na kuishirikisha katika uwekezaji, hususani ujenzi wa viwanda kwa kuimarisha Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini (Blue Print).

Majaliwa aliyasema hayo alipohutubia mkutano wa kampeni katika Kata ya Majengo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

Katika mkutano huo alimuombea kura mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, Rais John Magufuli, mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Priscus Tarimo na wagombea udiwani.

Majaliwa aliagiza viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro, waandae jukwaa maalumu kutangaza vivutio vya uwekezaji vilivyoko ndani ya mkoa huo ili kushawishi wawekezaji kwenda kuwekeza.

Alisema uwepo wa viwanda vingi utawezesha wananchi hususani vijana kupata ajira kwa sababu vinaajiri watu wengi. Pia aliwataka vijana kujishughulisha na shughuli zitakazowapatia kipato cha halali, badala ya kusubiri ajira kutoka serikalini.

Majaliwa alisema serikali ya CCM itaendelea kusimamia nidhamu kwa watumishi wa umma na kudhibiti vitendo vya rushwa ili wananchi wanufaike na kuifurahia nchi yao.

Alisema jukumu kubwa la watumishi wa umma ni kuwatumikia wananchi bila ubaguzi wa aina yoyote, hivyo aliwataka waendelee kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu.

Majaliwa aliwaomba wakazi wa Moshi na Watanzania wawachague wagombea wa CCM ili maendeleo yaendelee kupatikana katika maeneo yao.

"Nimekuja hapa kumuombea kura Rais Dk Magufuli. Hakikisheni ifikapo Oktoba 28, 2020 mnapofika katika vituo vya kupigia kura unachukua karatasi ya kupigia kura na kumchagua Rais Dk Magufuli kwa kipindi cha miaka mitano mingine. Mnafahamu vizuri kazi kubwa aliyoifanya miaka mitano iliyopita."alisema.

Majaliwa alisema, katika kipindi cha miaka mitano Serikali ya Rais Magufuli imeweza kuboresha huduma za afya kwa kujenga zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na mkoa ili wananchi wapate huduma bora za tiba.

Alitumia mkutano huo kukutanisha mgombea ubunge wa CCM jimbo la Moshi Mjini, Tarimo na mtia nia aliyeomba uteuzi, lakini hakuteuliwa, Ibrahim Shayo.

Shayo alitamka hadharani kuwa atamuunga mkono Tarimo ili kuhakikisha CCM inashinda.

Chanzo: habarileo.co.tz