Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sekta binafsi isaidie shughuli za uhifadhi

D5b4acfb4fda78d68317d287cc839931 Habari za uhifadhi hazipigiwi chapuo na vyombo vingi

Tue, 12 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

SEKTA binafsi ina nafasi kubwa katika kusaidia shughuli za uhifadhi nchini, ikiwa ni moja ya njia zinazolinda rasilimali zilizopo kwa manufaa ya kizazi kijacho.

Akizungumza jana jijini Dar es salaam katika mkutano wa Chama cha Waandishi wa habari za mazingira (JET), mchambuzi wa sera kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Victoria Michael, alisema sekta hiyo inahimizwa kushiriki shughuli hizo kuanzia michakato mbalimbali kwa manufaa ya taifa.

“ Ipo nafasi kwa sekta binafsi katika kusaidia uhifadhi nchini Tanzania, hata kuwezesha wahusika wa mnyororo wa thamani katika maeneo ya uwekezaji,” alisema Victoria katika mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao.

Mkutano huo unaratibiwa na JET na kufadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Misaada la Marekani (USAID) chini ya mradi wa Tuhifadhi Mazingira.

Alitolea mfano ushiriki wa TPSF katika uhifadhi kuwa ni pamoja na kushughulikia changamoto zinazohusiana na uhifadhi, lakini pia katika ushawishi wa sera mbalimbali zenye kulinda eneo hilo.

Alisema wamekuwa wakiratibu mijadala ya kijamii, huku wakishirikiana na wadau mbalimbali kuelimisha kuhusu sera ya uhifadhi nchini na hata fidia wapatazo waathiriwa wa majanga ya kuvamiwa na wanyamapori.

“Tunaendelea kujenga uelewa kwa sekta binafsi nchini, ili kila mmoja kutambua wajibu alionao katika kulinda na kuboresha uhifadhi nchini, lakini pia tukishirikiana na serikali,” alisema Victoria.

Alisema katika ushirikiano na wadau mbalimbali, TPSF inatetea mazingira wezeshi ya biashara kwa kuhamasisha mazingira bora ya uwekezaji endelevu, kupiga vita vitendo kama vya usafirishaji haramu wa wanyamapori na uharibifu wa hifadhi na mazingira.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Taasisi ya Uhifadhi ya Chemchem Association, Walter Pallangyo, alisema taasisi hiyo imeshiriki matukio mbalimbai katika kulinda uhifadhi, ikiwa ni hatua mojawapo za kuimarisha sekta hiyo.

Mkurugenzi wa JET, John Chikomo aliwataka waandishi kujikita kuandika kwa wingi habari za mazingira na uhifadhi kwa ujumla, jambo litakalosaidia kuibua changamoto zilizopo na fursa zilizopo pia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live