Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) inatarajia kutangaza zabuni za ujenzi wa bandari mpya ya Kisiwa Mgao mwezi huu.
Bandari hiyo itakuwa maalumu kuhudumia shehena ya bidhaa chafuzi yakiwamo makaa ya mawe, saruji, madini ya manganese, chuma kutoka Mchuchuma na Liganga na madini ya graphite yaliyoanza kuchimbwa wilayani Ruangwa mkoani Lindi.
Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara, James Ng’wandu amesema ujenzi wa bandari hiyo utachukua miaka miwili hadi mitatu. Bandari hiyo itajengwa kwenye eneo la hekta 25 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
“Ni eneo letu la muda mrefu na hati tayari tunayo na lipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara,’’ alisema Ng’wandu na akaongeza kuwa bandari hiyo itahudumia meli ya zaidi ya tani 100,000. Alisema ujenzi wa bandari hiyo ni kwa ajili ya shehena chafuzi na inalenga kulinda mazingira.
“Shehena ya makaa ya mawe imekuja na uchafuzi wa mazingira kunapokuwa na upepo mkali na wakati wa kiangazi hivyo tumeanza kuchukua hatua za kukabiliana na hali hiyo,” alisema Ng’wandu.