Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samia kufungua mkutano wa kimataifa wa madini

0cdfe938103093783f7541105dd661b2 Samia kufungua mkutano wa kimataifa wa madini

Sun, 21 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufungua Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini wenye lengo la kutangaza fursa za uwekezaji wa sekta hiyo nchini.

Taarifa ya Wizara ya Madini iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Waziri mwenye dhamana, Dotto Biteko, ilieleza kuwa mkutano huo utaanza leo hadi Februari 23 mwaka huu na utafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Ilieleza kuwa Makamu wa Rais atafungua rasmi mkutano huo kesho, Februari 22, mwaka huu. Mkutano huo unaofanyika kila mwaka kuanzia mwaka 2019, umebeba kauli mbiu isemayo: “Sekta ya Madini kwa Uchumi Imara na Maendeleo Endelevu”.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Waziri Biteko, mkutano huo utahusisha viongozi na wataalamu wa madini kutoka nchi mbalimbali na kampuni za madini za ndani na nje ya nchi.

“Utakwenda sambamba na maonesho ya shughuli za utafutaji, uchimbaji, uongezaji thamani, biashara ya madini na namna ya uchakataji wa madini ya ujenzi na ya viwandani,” alieleza Biteko.

Alisema kuwa pamoja na lengo kuu la kutangaza fursa za uwekezaji ili kupata wawekezaji katika shughuli za madini, mkutano huo pia utasaidia kupata maoni ya wachimbaji na wadau wengine ya namna ya kuboresha zaidi usimamizi wa sekta hiyo.

Pia utasaidia kuwaunganisha watumiaji wa madini (wenye viwanda) na wachimbaji wa madini.

“Katika nchi yetu kuna viwanda vingi vinavyotumia malighafi zinazotokana na madini, mwaka huu tumeona tuwaalike ili wakutane na wachimbaji na wajue kiasi gani cha malighafi hizo wanahitaji na kwa ubora gani,” ilieleza taarifa hiyo.

Pia mkutano utasaidia kuwaunganisha wachimbaji na watoa huduma katika shughuli mbalimbali zinazofanyika migodini, kuutangazia ulimwengu kuwa Tanzania kuna mazingira mazuri ya kuwekeza, uwepo wa madini mbalimbali na kutoa elimu kwa wadau kuhusu sekta na sheria zake.

“Mwaka huu tumeona tutoe tuzo kwa wadau ambao wamefanya vizuri katika kutekeleza sheria zinazosimamia sekta ya madini, mfano tutamtambua mlipa kodi mzuri anayefanya vizuri katika CSR (Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii) n.k,” alisema Biteko katika taarifa hiyo.

Alisema ili kuhakikisha mausala ya uongezaji thamani madini hapa nchini ikiwemo kuwafanya Watanzania kutumia bidhaa za mapambo ya madini ya vito yanayopatikana nchini, wameandaa maonesho maalum ya bidhaa hizo za mapambo kueleza kuwa vitu hivyo vipo na vinatengenezwa na Watanzania hapa hapa nchini.

Biteko alisema sambamba na maonesho hayo maalumu ya vito, kutakuwa na maonesho ya madini yanayoanza leo sambamba na mkutano huo.

Aliwakaribisha wananchi kujionea maonesho ya madini, wajionee madini mbalimbali yanayopatikana nchini ikiwemo kujua namna shughuli za uchimbaji madini zinavyofanyika hasa ikizingatiwa kuwa zipo kampuni kubwa, za kati na ndogo zinazofanya kazi hiyo na zinashiriki maonesho hayo.

*********

Chanzo: habarileo.co.tz