Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samia azipa benki fursa kilimo cha umwagiliaji

Samia Pic Samia azipa benki fursa kilimo cha umwagiliaji

Mon, 7 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais Samia Suluhu amezitaka taasisi za kifedha nchini kuiwezesha sekta binafsi ishiriki katika kilimo, hasa cha umwagiliaji ambacho Serikali ndiyo kipaumbele chake kwa mwaka ujao wa fedha.

Rais hiyo ameitoa juzi jijini Dar es Salaam, wakati wa akizindua jengo la makao makuu ya benki ya CRDB lililojengwa karibu na barabara ya Ali Hassan Mwinyi kwa gharama ya Sh163 bilioni.

“Mwakani tunaweka kipaumbele kwenye kilimo cha umwagiliaji. Juzi nilikuwa Ubelgiji, wanakula mchele kutoka Tanzania, kwa hiyo kama tutaweka miundombinu ya umwagiliaji na kuwafanya wakulima watumie miundombinu hiyo, wavune mara mbili kwa mwaka,” alisema Rais Samia.

Alisema Serikali imeamua kukipa kilimo kipaumbele kwa kuwa hili ndilo eneo ambalo litawapa wananchi mapato ya haraka.

“Tusafishe kwa standard zilizowekwa na tusafirishe mchele wetu Ulaya kwa wingi, hilo eneo litatupa hela nyingi,” alisema Rais Samia.

Hata hivyo, alisema sio mchele peke yake, hata mbogamboga kwani hivi karibuni alipokuwa Falme za Kiarabu, walisaini mkataba mkubwa ambao zaidi ya tani 60 za mboga zinatakiwa kwa mwaka.

“Baada ya kusaini mkataba ule, nikashtuka nikasema tutaweza kweli, kwa hiyo tukitumia kilimo cha umwagiliaji maji, tukawafanya vijana wetu wajiajiri kwenye kilimo cha mpunga au mbogamboga tutapata mapato ya haraka,” alisema.

“Naomba litupieni macho sana hilo, CRDB pamoja na umoja wenu wa mabenki muweze kulifanyia kazi hilo,” alisema Rais Samia.

Rais Samia pia alizitaka benki nchini kuwekeza katika kujenga majengo kwenye viwanja vilivyopo katika balozi mbalimbali za Tanzania nje ya nchi.

Alisema anajua benki zina uwezo huo, hivyo alimpa jukumu Mkurugenzi wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, kupitia umoja wao wa mabenki, kwenda kuwahamasisha wenzake kufanya hivyo.

“Naomba niwadokeze kipengele kingine ambacho mnaweza kuwekeza, jana tulikuwa na mkutano wa bajeti, tulijadili bajeti yetu lakini tukakuta kwenye Wizara ya Mambo ya Nje kuna viwanja vingi vipo nje ya nchi ambavyo ni mali yetu, lakini Serikali inashindwa kuvijenga, naomba tumieni hiyo kama fursa ya uwekezaji, nendeni mkajenge majengo kule, mkodishe, mfanye biashara zenu ili viwanja vile tusiendelee kunyang’anywa,” alisema.

Benki zinafufuka

Katika hafla hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisema tangu Rais Samia aingie madarakani taasisi za kifedha zilianza kufufuka kutokana na hatua za makusudi zilizochukuliwa.

“Umesaidia sana kufufua taasisi za kifedha, ilikuwa haisemwi tu kwa sauti kubwa, lakini hali ilikuwa mbaya, pumzi ilikata, sera na hatua ulizozichukua tangu uingie madarakani zimesaidia kunusuru hali hiyo,” alisema Dk Mwigulu.

Alisema agizo la kulipwa kwa madeni ya ndani lilisaidia kuleta uhai kwa taasisi za fedha kwa kuwa baadhi ya wazabuni waliokuwa wakiidai Serikali nao walikuwa wanadaiwa na taasisi hizo, hivyo walipolipwa nao wakalipa madeni yao.

Dk Mwigulu alisema utekelezaji wa miradi mbalimbali katika ngazi tofauti na juhudi za kuendelea kuvutia uwekezaji wa ndani na nje navyo vimeongeza mzunguko wa fedha, hivyo kuleta uhai kwa taasisi za kifedha.

Baada ya kueleza hayo, Mwigulu alitoa rai kwa Watanzania wote kuwa na utamaduni wa kuweka fedha zao benki, huku akisema Serikali ina dhamira ya kulinda wafanyabiashara na biashara zao.

“Wakopaji tuheshimu mikopo hasa wanaume, tunapochukua mikopo tutathmini vizuri, itumike vizuri kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuweza kurejesha,” alisema Dk Mwigulu.

Alikemea tabia ya taasisi za fedha kutamani dhamana ya mteja kwa kuuza mali yake pindi anaposhindwa kufanya marejesho kwa muda. “Wakati Mwingine unakuta mtu alikuwa anakaribia kumaliza mkopo huo au deni lililobaki ni dogo haliendani na thamani ya dhamana,” alisema.

Kauli ya BoT

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Profesa Florens Luoga alisema kinachotokea sasa kinathibitisha kuwa benki za Tanzania zimeimarika na hata wakati wa mlipuko wa janga la Uviko-19 sekta ya fedha Tanzania haikuathirika.

“Wakati wa Uviko-19 Tanzania ni nchi ambayo sekta ya fedha haikuathirika, tuliisimamia vizuri, tuliamini kuwa baada ya janga hilo sekta ya benki itategemewa kufufua uchumi na biashara,” alisema Profesa Luoga.

Luoga aliongeza kuwa nchi mbalimbali zimeonyesha nia ya kutaka benki za Tanzania kwenda kufungua matawi nchini mwao kutokana na kuvutiwa na huduma zao zinazotolewa hapa nchini.

“Ni lazima tuchukue hii nafasi kwenda kutoa huduma kule nje, hii itasaidia benki za Tanzania ziwe mfano katika nchi za Afrika Mshariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC) katika utoaji huduma,” alisema.

CRDB kujitanua

Naye Mkurugenzi wa CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema wamefungua tawi nchini Burundi na Congo DRC watafungua siku chache zijazo, huku pia wakilenga kwenda nchi nyingine tano.

Kuhusu jengo hilo, Nsekela alisema lina ofisi za kisasa za kuwawezesha wafanyakazi kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi na kwa tija.

“Jengo hili kinatoa nafasi kwa wafanyakazi kushirikiana na kupumzika pindi wanapokuwa wamechoka, hii inawapa uwezo wa kuwa wabunifu zaidi. Lina vyumba 60 vya mikutano na kipo ambacho kinaweza kuchukua hadi watu 200. Mteja wetu anapewa chumba cha mikutano bure kuzungumza na wateja wake,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live