Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wafanyabiashara wa Oman kuja kuwekeza nchini na kutaja fursa zilizopo kuwa ni uwekezaji kwenye kilimo, mifugo, uvuvi, madini, utalii, uzalishaji, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na maendeleo ya miundombinu.
Pia ametaja sababu za wawekezaji kuwekeza nchini kuwa ni mazingira mazuri ya uwekezaji, utawala bora, soko la kutosha linalofikia watu bilioni 1.3, mikataba inayolinda wawekezaji, umeme, miundombinu, maji na ardhi ya kutosha.
Rais Samia aliyasema hayo Muscat nchini Oman jana aliposhiriki katika Kongamano la Wafanyabiashara wa Oman na Tanzania pamoja na kushuhudia utiaji saini Makubaliano ya Ushirikiano wa Pamoja katika sekta mbalimbali, akiwa katika ziara ya kikazi ya kiserikali.
Alisema katika eneo la kilimo, kuna ardhi ya kutosha ambayo haijatumika kwa uwekezaji ambako pia kwa Tanzania kilimo kinagusa maeneo mengine mawili ya uwekezaji ambayo ni mifugo na uvuvi.
Alisema katika kilimo ambako bado uwekezaji wake nchini si mkubwa, kuna maeneo mengi ikiwamo kilimo cha umwagiliaji.
“Katika madini, takribani madini yote yanayopatikana duniani yanapatikana pia Tanzania. Lakini tumebarikiwa Mungu ametupa madini ambayo hayapatikani popote duniani, bali Tanzania ambayo tanzanite,” alisema Rais Samia.
Aidha, alisema kwa sasa Tanzania inataka kuanza kujikita katika uchumi wa gesi baada ya kubaini uwapo wa gesi nyingi na hivi karibuni itakuwa ni moja ya sehemu inayozalisha gesi hiyo duniani.
Aidha, alisema Tanzania pia imebarikiwa katika eneo la asili ambako kuna vivutio vingi vya utalii ikiwamo kisiwa cha historia cha Zanzibar na mbuga za wanyama maarufu duniani ambako kote huko kuna fursa nyingi za uwekezaji ikiwamo ujenzi wa hoteli za kitalii.
“Tunahitaji hoteli zaidi za kitalii, tuna wingi wa watalii wanaokuja nchini na hoteli zilizopo hazitoshi. Naomba mje muwekeze na eneo hili,” alisisitiza.
Aidha, alisema pia Tanzania imebarikiwa kuwa na maziwa makubwa na eneo kubwa la bahari, uvuvi ni fursa nyingine inayopatikana nchini humo ambapo kwa sasa hakuna uvuvi mkubwa nchini kwetu. “Hili ni eneo ambalo tunaweza kulifanyia kazi kwa pamoja,” alieleza.
Pamoja na hayo, Rais Samia alitaja sababu za wafanyabiashara wa Oman kuwekeza nchini kuwa ni pamoja na uhusiano wa kitamaduni na udungu wa kihistoria wa damu.
“Huwezi kuharibu biashara za kaka na dada zako. Sisi ni ndugu wa damu, kaka na dada. Pia historia yetu inaanzia karne ya 19 hali inayotoa uaminifu na kujiamini kwamba uwekezaji wenu uko mahali salama,” alisisitiza.
Pia, alisema sababu nyingine ya kuwekeza Tanzania ni amani na utulivu na utawala bora. “Niko hapa, mimi ndio kiongozi wa nchi ninachozungumza kinatoka mdomoni na moyoni kwangu kwamba tuna serikali inayozingatia utawala bora, njooni muwekeze,” alisema.
Aidha, alisema Tanzania ni mwanachama wa jumuiya na makubaliano mbalimbali. Ni mwanachama wa Wakala wa Bima ya Biashara ya Afrika, ni mwanachama wa mashirika ya kimataifa yanayohusika na usuluhishi hivyo endapo kutakuwa na tatizo la kiuwekezaji, wawekezaji wana sehemu ya kwenda kusuluhishwa.
Alisema Tanzania ina uchumi imara na sera ya fedha thabiti na ni moja ya nchi ambayo uchumi wake unakua kwa kasi Afrika.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Dunia ya Masuala ya uchumi pamoja na athari kubwa za janga la Covid 19, uchumi wa Tanzania ulikuwa na kuongoza katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Viashiria vyote vidogo vya uchumi ni vizuri pamoja na janga hilo na ukuaji wa Pato la Taifa ulikuwa wastani wa asilimia 6.7. lakini kutokana na Covid-19 tulishuka hadi asilimia nne, lakini sasa tunazungumzia ukuaji wa asilimia tano tuko vizuri,” alisisitiza.
Alisema serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuinua sekta binafsi
“Tangu niingie madarakani sera yangu ni kuiacha serikali iongoze na sekta binafgsi ifanye biashara. Na nina maanisha, hakuna serikali kufanya biashara tuiachie sekta binafsi kufanya biashara. Sisi serikali tutatengeneza mazingira mazuri kwa sekta binafsi wawe wa ndani au wa nje kufanya biashara,” alieleza.
Alisema serikali imefanya jitihada kubwa za kupunguza misururu ya kodi na usimamizi wa mamlaka nyingi kwa wafanyabiashara.
Aidha, Tanzania ina fursa nzuri ya masoko ambapo ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye zaidi ya watu milioni 300, mwanachama wa Jumuiya wa Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa pamoja ina watu milioni 500 na ni mwanachama wa Eneo Huru la Afrika na hivyo kufanya kuwa na soko linalofikia watu bilioni 1.3.
“Jambo zuri zaidi Tanzania ni mlango wa nchi hizo zote za Afrika kwa hiyo ukifanya biashara na Tanzania umefanya biashara Afrika nzima. Pia, tuna nguvu kazi ya kutosha na idadi kubwa ya Watanzania ni vijana ni kama asilimia 65 ya Watanzania wote,” alisema.
Akizungumzia biashara baina ya Oman na Tanzania, alisema biashara baina ya nchi hizo ilianza karne na mtiririko wa biashara na uwekezaji unazidi kukua ingawa bado uwiano wake hauridhishi.
Alisema katika miaka mitano iliyopita kuanzia 2017/21 wastani wa thamani ya biashara ilikuwa dola za Marekani milioni 112. 3 ambapo wastani wa thamani ya Tanzania kuuza nje kwenda Oman ni dola za Marekani milioni 6.4 na kuagiza kutoka Oman ilikuwa dola za Marekani milioni 105.
“Kwa hiyo kiwango cha biashara kinaweza kuinuliwa, yapo mambo mengi tunaweza kufanya kuinua kiwango cha biashara baina yetu, takwimu zinaonesha hakuna uwiano mzuri. Zinaonesha Oman inafanya vizuri zaidi kuliko Tanzania,” alisisitiza.
Kwa upande wa sekta ya uwekezaji, alisema kiwango cha uwekezaji kimekua juu kwa upande wa Tanzania. Hadi kufikia Aprili 2022, Tanzania imesajili miradi 62 ya uwekezaji yenye thamani ya dola za Marekani milioni 308.35 na kutengeneza kiasi cha 2,400 ajira.
Alisema uwekezaji huo ni kwa sekta kilimo, majengo ya biashara ya mali isiyohamishika, ujenzi, rasilimali watu, utalii, uzalishaji, uchukuzimawasiliano ya simu na maendeleo ya miundombinu.
Alisema Tanzania inatambua jukumu kuu la uwekezaji katika kuleta ukuaji wa uchumi na ajira. Katika kuvutia uwekezaji wa ndani na wa nje imejitahidi kufanya sera zake ziwe rafiki zaidi katika uwekezaji na biashara.
“Najua kumekuwa na baadhi ya changamoto lazima nitambue hili kumekuwa na changamoto na kukatisha tamaa lakini mimi niko hapa na chukueni maneno yangu kwamba naenda kusahihisha mambo yote yaliyotokea huko nyuma na sasa tunaenda kufanya kazi, kufanya biashara na kuwekeza pamoja,” alieleza.
Alisema pamoja na kuelezea fursa zinazopatikana Tanzania kwa wafanyabiashara wa Oman, ni vyema pia wafanyabiashara wa Tanzania nao kuangalia ni mambo gani wanaweza kufanya pamoja na wafanyabiashara wenzao kwa ushirikiano wa serikali zote mbili.
Kuhusu mazingira mazuri ya uwekezaji, Rais Samia alisema nchi inazidi kujiimarisha kwa kuboresha miundombinu na kutolea mfano ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), uzalishaji umeme wa kutosha kupitia Mradi wa Julius Nyerere ambao ukikamilisha nchi itakuwa na megawati za umeme takribani 10,000 na miradi mbalimbali ya maji.
Naye Waziri wa Biashara na Viwanda wa Oman, Qais bin Mohammed Al Yousef alipongeza kasi ya ukuaji wa uchumi Tanzania na kueleza namna kongamano hilo litajadili fursa hizo za biashara na uwekezaji ambazo ni kilimo, uvuvi, madini na utalii kwa manufaa ya pande zote.