Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samia atoa maagizo 4 biashara na Rwanda

142d0d945384c096a32d327f717d209c.jpeg Samia atoa maagizo 4 biashara na Rwanda

Fri, 4 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

RAIS Samia Suluhu Hassan ameiagiza Tume ya Pamoja ya Ushirikiano wa Tanzania na Rwanda (JPC) kukutana ili kuongeza msukumo wa ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili ukiwemo ushirikiano wa kibiashara na miradi ya pamoja.

Alitoa maagizo hayo jana Ikulu Dodoma baada ya kupokea ujumbe kutoka kwa Rais wa Rwanda, Paul Kagame, uliowasilishwa kwake na Mjumbe Maalumu na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Rwanda, Dk Vincent Biruta.

Taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari jana, ilisema Rais Samia pia ameitaka tume hiyo kukutana ili kuongeza msukumo katika utekelezaji wa miradi ya pamoja ukiwemo wa kuzalisha umeme wa Rusumo.

Mradi huo unahusu ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa MW 80 kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Kagera. Mradi huo unazihusisha nchi tatu za Tanzania, Burundi na Rwanda.

Juzi Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemami aliwaeleza wabunge kuwa, kwa upande wa Tanzania mradi huo unahusu pia ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kV 220 kutoka Rusumo hadi Nyakanazi.

Alisema gharama za mradi wa kuzalisha umeme kwa upande wa Tanzania ni Dola za Marekani milioni 113 sawa na takriban Sh bilioni 265.9 kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.

Kalemani alilieleza Bunge kuwa, katika mwaka 2020/21 kazi zilizofanyika ni pamoja na kukamilika kwa uchimbaji wa eneo la kusimika mitambo, milango ya kuingiza na kuchepusha maji na ujenzi wa nyumba za wafanyakazi.

Alitaja kazi zinazoendelea kuwa ni pamoja na uchimbaji wa handaki la kupitishia maji; ufungaji wa mitambo na ujenzi wa kituo cha kuongeza nguvu ya umeme.

Kwa mujibu wa Dk Kalemani hadi sasa utekelezaji wa mradi kwa jumla umefikia asilimia 80.

Alisema kazi zilizopangwa kufanyika mwaka 2021/2022 ni pamoja na kukamilisha uchimbaji wa handaki la kupitishia maji, ufungaji wa mitambo, ujenzi wa kituo cha kuongeza nguvu ya umeme na utekelezaji wa miradi ya kijamii kwa upande wa Tanzania.

Fedha za nje Sh bilioni 3.85 zimetengwa katika mwaka 2021/22 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za mradi huu unaotarajiwa kukamilika Desemba, 2021.

Rais Samia aliitaka tume hiyo pia iongeze msukumo katika ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ya kuunganisha Jiji la Kigali nchini Rwanda na Isaka mkoani Shinyanga itakayosaidia usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Rwanda.

Aliitaka JPC kuainisha maeneo mapya ya ushirikiano yenye maslahi kwa pande zote mbili pamoja na kuimarisha usafirishaji wa minofu ya samaki kutoka Mwanza kupitia Shirika la Ndege la Rwanda na kuharakisha ujenzi wa Bandari Kavu ya Isaka.

Kupitia ujumbe huo, Rais Kagame pia alituma salamu za pole kwa Rais Samia kutokana na kifo cha Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Hayati John Magufuli kilichotokea Machi 17, mwaka huu.

Kagame pia amempongeza Samia kwa kuwa Rais wa Tanzania na amemhakikishia kuwa Rwanda ipo tayari kukuza uhusiano na ushirikiano na Tanzania.

Chanzo: www.habarileo.co.tz