Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samia ataka usalama wa chakula SADC

Ee700639189b63bcf1cd8cb31ede2b72.jpeg Samia ataka usalama wa chakula SADC

Fri, 19 Aug 2022 Chanzo: Habarileo

Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa usalama wa chakula katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), na kuzisihi nchi hizo kuwekeza kwenye uchumi wa buluu.

Rais Samia amependekeza hayo katika Mkutano wa 42 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika Kinshasa Mji Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) juzi.

Akizungumzia uwiano wa kijinsia waliokubaliana katika ukanda huo, Rais Samia alisema Tanzania imejitahidi kutoa fursa kwa wanawake hasa katika nafasi za uongozi za kimkakati. Miongoni mwa nafasi hizo za uongozi serikalini na bungeni ni pamoja na za uwaziri wa Ulinzi, Mambo ya Nje, Uwekezaji, Utalii pamoja na nafasi ya Spika wa Bunge.

Rais Samia alitoa maoni yake kwa lugha ya Kiswahili ikiwa ni jitihada za kuchapusha matumizi ya lugha hiyo miongoni mwa nchi za SADC.

Katika mkutano huo uliopitisha maazimio 27, Rais Samia amesisitiza uharakishwaji wa mchakato wa Kiswahili kupitishwa rasmi kama lugha ya nne ya SADC. Mkutano huo wa SADC pia ulishuhudia makabidhiano ya Uenyekiti kutoka kwa Rais wa Malawi, Dk Lazarus Chakwera na sasa nafasi hiyo imechukuliwa na Rais wa DRC, Felix Tshisekedi.

Aidha, Rais Samia jana alifanya ziara ya kikazi ya siku moja nchini DRC ambako pamoja na mambo mengine, atafanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Tshisekedi. Maazimio hayo 27 yaliyopitishwa na mkutano huo ni kuanzishwa kwa Kituo cha Kupambana na Ugaidi (SADC-RCTC) nchini Tanzania.

Pia, mkutano uliidhinisha uteuzi wa Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete kuwa Mwenyekiti wa Jopo la Wazee (POE) na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Mauritius, Paramasivum Pillay kuwa Naibu wa Mwenyekiti wa jopo hilo.

Mkutano huo pia uliidhinisha kuanzishwa kwa Kamati ya Uangalizi inayoundwa na Jopo la Wazee la SADC (PoE) na Kikundi cha Upatanishi (MRG) ili kuhakikisha kunakuwa na uangalizi katika utekelezaji wa mageuzi katika Ufalme wa Lesotho.

Aidha, uliridhia na kusaini mikataba mbalimbali ukiwamo Mkataba wa Mabadiliko ya Jukwaa la Wabunge wa SADC kuwa na Bunge la SADC; na Mkataba wa Kurekebisha Itifaki ya Maendeleo ya Utalii SADC. Pia, ulipitisha Mkataba wa Makubaliano kati ya nchi wanachama kuanzisha Kituo cha Shughuli za Kibinadamu na Dharura na kukabidhi kwa mawaziri wanaohusika na maafa kwa ajili ya kuusaini.

Aidha, mkutano huo ulipitisha na kusaini Itifaki dhidi ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu, kupitisha mfumo wa ushirikiano katika kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu na wanaohusishwa na uhalifu wa kimataifa katika jumuiya hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jumuiya hiyo, mkutano huo pia ulipokea ripoti mbalimbali za utekelezaji ambazo ni ripoti ya Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa Chombo cha Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini.

Mkutano huo ulimpongeza kwa uongozi wake bora na kuendeleza juhudi za kukabiliana na matishio ya amani na usalama katika mwaka huu, licha ya changamoto zinazoletwa na Covid-19. Ripoti nyingine ni kutoka kwa Mwezeshaji wa SADC hadi Ufalme wa Lesotho, Ramaphosa kwenye utekelezaji wa maamuzi ya SADC katika ufalme huo, inayobainisha hatua iliyofikiwa.

Ripoti hiyo iliitaka Serikali ya Lesotho kuharakisha kukamilisha mageuzi yanayoendelea, na kuendelea na amani na mchakato wa maridhiano ili kuleta umoja wa kitaifa na mshikamano wa kitaifa.

Halikadhalika, mkutano huo uliridhia ripoti fupi iliyotolewa na Serikali ya Ufalme wa Eswatini, kuhusu hali ya usalama nchini humo ambayo pia ililaani kuhusu vurugu zilizojitokeza na kuamuru hatua zaidi kuchukuliwa ili kutafuta suluhu na amani katika nchi hiyo.

SADC pia ilipokea ripoti ya maendeleo ya utekelezaji wa Utaratibu wa Kuheshimu Waasisi wa SADC na kutambua urithi na mchango wao.

Aidha, ilikabidhi nishani kwa wawakilishi wa waasisi tisa wa jumuiya hiyo na kumuagiza Mwenyekiti wa chombo hicho kuratibu mchakato wa kuzindua sanamu kwa kumbukumbu ya Rais Julius Nyerere katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU), Addis Ababa, Ethiopia.

Mkutano ulipokea taarifa kuhusu hali ya usalama eneo la Cabo Mkoa wa Delgado, Kaskazini mwa Msumbiji, na kuidhinisha kuongezewa muda kwa Ujumbe wa SADC Msumbiji (SAMIM) na taratibu zake.

Pamoja na hayo, mkutano huo ulionesha wasiwasi na mshikamano juu ya usalama wa DRC na kumpa mamlaka Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri, kushirikisha na Umoja wa Mataifa (UN) kuchunguza njia zote za kusaidia juhudi kuelekea kuboresha hali ya usalama.

Chanzo: Habarileo