Wafanyabiashara na wadau wa maendeleo nchini wametakiwa kutumia fursa ya mashindano ya soka Kombe la Dunia yanayotarajiwa kufanyika mwakani, nchini Qatar ili kujiinua na kuinua nchi kiuchumi.
Rais Samia Suluhu Hassan alisema hayo jana Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akizungumza baada ya kupokea kombe la ushindi la Michuano ya Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati kwa vijana wenye umri chini ya miaka 23.
Alisema Qatar si mbali na Tanzania hivyo wafanyabiashara, sekta binafsi, serikali na wadau wote wa maendeleo wajiandae kuitumia fursa hiyo kibiashara ili kukuza uchumi.
“Tunajua Qatar itaingiza watu wengi sana kutoka dunia yote, na wanataka vitu vingi, kuanzia vyakula na mambo mengine. Tujipange sekta binafsi na sisi serikali pamoja na wadau wengine tuone jinsi ya kutumia michezo hiyo ili nchi nayo ipate kidogo,” alisema Rais Samia.
Alisema katika utalii inawezekana kutengeneza vifurushi maalumu ili watu wanaoenda Qatar badala ya kurudi kwao waje kutalii nchini.
“Watumie tiketi hiyo hiyo waliyonayo kwa package ndogo waje kuangalia mambo yetu Tanzania. Lakini niombe sana wafanyabiashara wakati huo, mambo mengi yatahitajika Qatar tutumie nafasi hiyo,” alisema Rais Samia.
Alisema Watanzania ni wazalishaji wa korosho na katika kipindi hicho korosho zitatakiwa Qatar.
“Tuone jinsi tutakavyo ipack (uwekaji katika vifungashio) vizuri na kutafuta soko la kupeleka huko badala ya kutegemea masoko ambayo tunayo siku zote. Hili ni soko jipya na litakuza sana bei ya korosho zetu. Lakini pia hata nyama, samaki na mambo mengine tuangalie,” alisema Rais Samia.
Kombe la Dunia linatarajiwa kufanyika Novemba 21 hadi 18 Desemba mwakani likishirikisha timu 32 za taifa za nchi zitakazofuzu.
Mashindano hayo hufanyika kila baada ya miaka minne. Mwaka 2018 yalifanyika Urusi.