Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samia ataka fursa za China ziletwe nchini

3ef12599436fd87a25c9d6b1b0152e5e.jpeg Samia ataka fursa za China ziletwe nchini

Tue, 10 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania wanaoishi na kufanya biashara China kubaini fursa za kiuchumi zilizopo huko na kuzilete nchini ili ziwanufaishe Watanzania.

Ili kufanikisha hilo, Ubalozi wa Tanzania nchini humo unapanga kuanzisha Dawati la Viwanda ili kuwezesha Watanzania wanaohitaji teknolojia kutoka China.

Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki alisema hayo alipozungumza na Watanzania wanaoishi na kufanya biashara nchini China.

Katika mkutano huo kwa njia ya mtandao, Balozi Kairuki alisema uhusiano wa Tanzania na China umezidi kuimarika na ndani ya siku 100 za Rais Samia tangu aingie madarakani, alizungumza na Rais wa China, Xi Jinping na kukubaliana kuuimarisha katika nyanja za uchumi na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Covid-19.

Aliwaeleza kuwa Rais Samia anawatakia kila la kheri katika majukumu yao na anatarajia kuwa wanaelewa anayosisitiza ikiwemo rai kwa Watanzania washiriki katika shughuli za uchumi.

“Rais Samia amesema anajua kwamba China ni kitovu cha uchumi, ni ya pili kwa ukubwa wa uchumi duniani, kwa hiyo zipo fursa nyingi na ni mategemeo yake kwamba, ninyi mliopo huku mtakuwa macho kuziangalia fursa hizo na kuzipeleka nyumbani ili nchi yetu iweze kunufaika,” alisema Balozi Kairuki.

Aliwaeleza kuwa nchi ipo shwari na Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea na ujenzi wa taifa na mkazo uliopo ni kuuhami uchumi unaokabiliwa na changamoto ya Covid-19.

DAWATI LA VIWANDA

Balozi Kairuki alisema ubalozi huo unapanga kuanzisha Dawati la Viwanda kwa sababu ya ongezeko la Watanzania wanaoomba msaada wa ubalozi kuwaunganisha na wazalishaji wa mashine hasa kipindi ambacho mipaka ya China imefungwa na hawawezi kusafiri kwenda China.

“Kwa hiyo tutakuwa na ofisa ambaye kazi yake ni uratibu, na niweke bayana kwamba si dhamira ya ubalozi kufanya biashara ya kununua mizigo au kusafirisha mizigo, bali kazi ya ubalozi ni kuratibu,” alisema.

Balozi Kairuki alisema kwa kutumia dawati hilo, Mtanzania akipata kampuni kwa njia yoyote ikiwemo ya kuambiwa na mtu mwingine au kwa mtandao, anaweza kuuomba ubalozi uchunguze kubaini kama kampuni hiyo ina uwezo na sifa zinazostahili.

“Ubalozi tuna wajibu wa kumpa mtu huyo taarifa kwa sababu tuna mfumo unaotuwezesha kuangalia kampuni zote zilizopo hapa China, sifa na uwezo wao au kama zina mashitaka mahakamani,” alisema.

Kwa mujibu wa Balozi Kairuki, kwa kuwa bidhaa zinapatikana kidijiti, mtu anaweza kuuomba ubalozi uufuatilie mtandao husika ili kujiridhisha kama ni salama na sahihi.

Alibainisha kuwa, kundi la tatu la wanaoweza kunufaika na dawati hilo ni watu wanaotaka kununua mashine za viwandani kutoka China.

Alisema ubalozi utashirikiana na jumuiya ya wafanyabiashara wa Tanzania waliopo China kusaidia kuorodhesha kampuni zenye uzoefu wa kufanya kazi hiyo.

“Hii ni fursa kwa Watanzania mnaofanya shughuli zenu hapa kupanua soko lenu, kwa sasa mnafanya shughuli hizi lakini hamfahamiki,” alisema,

Akaongeza: “Rai yetu kwenu mjipangeni vizuri, tuzibainishe kampuni zinazofanya kazi hizi ambao ni waaminifu, waadilifu, wana kumbukumbu nzuri ya kufanya kazi bila kulalamikiwa, tunaomba mtoe ushirikiano kwa jambo hili.”

Chanzo: www.habarileo.co.tz